Mashabiki wa Arsenal wakamatwa

Dar es Salaam. Polisi mjini Jinja nchini Uganda wamewashikilia takriban wafuasi 20 wa klabu ya Arsenal ya Ligi Kuu England, kutokana na kuanzisha gwaride la kushangilia ushindi katika mitaa ya jiji hilo kutokana na kichapo walichokitoa kwa wapinzani wao Manchester United, ambapo mabao yalikuwa 3-2.
Mashabiki hao walikamatwa jana Januari 22, 2023 baada ya ushindi dhidi ya Manchester wakipiga gwaride la kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu England katika Jiji la Jinja nchini humo.
Polisi walikamata kundi la mashabiki wa hao waliokuwa na furaha waliokuwa katika msafara wa magari matano walipokuwa wakijaribu kuingia Barabara ya Iganga kutoka barabara kuu.
Wakati Polisi wakiwa hawajazungumzia tukio hilo, Baker Kasule ambaye alikuwa katika kundi hilo, alikieleza kitu cha habari cha Daily Monitor, kuwa gari la askari wa doria lilisimama mbele yao na kuwataka kila mmoja kushuka na kupanda gari la doria lililokuwa likielekea Jinja, katika kituo cha polisi.

"Sijui tumefanya nini lakini tulikuwa tukisherehekea ushindi wetu dhidi ya wapinzani wetu Manchester United," alisema mmoja wa mashabiki hao, Kasule na kuongeza kuwa "ni wafuasi 20 kwa jumla tuliokamatwa katika Jiji la Jinja."

Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Polisi cha Jinja, Maurice Niyonzima, alikataa kuzungumzia suala hilo, akisema jeshi hilo lina msemaji.