Mastaa 10 waliopiga shoo ya kibabe CRDB Taifa Cup

Muktasari:

  • Msimu huu mashindano hayo yataanza kutimua vumbi rasmi Novemba 5-14, 2021 kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, ambapo makocha wameanza kuzinoa timu zao tayari kwa kuonyeshana ubavu.

Dar es Salaam. Baada ya kushuhudia Klabu Bingwa ya mchezo wa kikapu yaliyofanyika Arusha katika viwanja vya uhasibu na ABC kuibuka mabingwa, sasa uhondo wa burudani unarejea tena Dodoma.

Wapenzi wa mchezo wa kikapu kuanzia Novemba 5 hadi 14, mwaka huu katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma watashuhudia mashindano ya mpira wa kikapu 'CRDB Taifa Cup' ambapo timu 32 zitapima ubavu kusaka mbabe wa Taifa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela katika uzinduzi wa mashindano hayo mapema mwezi huu, alisema dau la udhamini limeongezeka kutoka Sh200 milioni msimu uliopita hadi Sh300 milioni msimu huu.


“Tumeona tuongeze zawadi mwaka huu ili kuongeza ushindani kwa timu na vijana watakaoshiriki. Tunaamini kuongezeka kwa zawadi kutaongeza motisha kwa vijana kuonyesha vipaji vyao,” amesema.


Wakati maandalizi kwa timu zote za mikoa zinazoshiriki yakiendelea kwa kasi, hapa tunakupa dondoo za wachezaji 10 waliotamba msimu uliopita. Katika mashindano hayo Mbeya walitangazwa wafalme kwa kuichapa Temeke kwa pointi 68 kwa 55.

Rehema Silomba - Temeke
Mchezaji Bora wa Kike

Nyota huyu upande wa wanawake katika ambaye alibeba tuzo ya mchezaji bora kwa wanawake (MVP) akiisaidia Temeke kucheza fainali.
Kushinda kwake tuzo hiyo na kuwabwaga nyota wengine, Rehema alibeba kitita cha Sh300,000 kama zawadi. Rehema anasifika zaidi kwa uwezo wake wa kuchezesha timu na kufunga pointi nyingi.

Baraka Sadick - Mbeya
Mchezaji Bora wa Kiume


Upande wa tuzo ya mchezaji bora wa kiume (MVP) ilikwenda kwa staa huyo wa Mbeya ambao ndio waliibuka mabingwa kwa kuichapa Temeke kwa pointi 68 kwa 55.

Baraka katika mchezo huo kwa lugha nyepesi ya watu wa mchezo wa kikapu tunaweza kusema aliiteka 'shoo' ya mchezo siku hiyo.
Katika mechi zote mbili za fainali, upande wa wanaume, Baraka alikuwa nyota wa mchezo aliyeongoza kwa kufunga pointi 20, kati ya pointi hizo alifunga katika maeneo ya mitupo mitatu mara tatu, akifuatiwa na Mwalimu Heri aliyefunga pointi 15.

Jesca Julius - CRDB
Mfungaji Bora wa Kike


Kama wewe ni mpenzi wa kikapu basi hili jina sio geni kwani, moja ya wachezaji wenye sifa za kipekee kwenye mchezo huu na msimu uliopita aliitumikia timu ya CRDB.
Katika mashindano ya msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa jumla akizoa pointi 153 na kuisaidia timu yake kufanya vyema katika mashindano hayo.

Tyrone Andrew- Tanga
Mfungaji Bora wa Kiume


Moja ya mikoa yenye sifa kubwa katika mchezo wa kikapu Tanzania unapoitaja basi huwezi kuacha kuutaja Mkoa wa Tanga, Dar es Salaam, Arusha na Mbeya.
Tyrone alitisha sana huyu jamaa msimu uliopita alipoiwakilisha vyema Tanga katika mashindano hayo akishinda tuzo hiyo ya ufungaji bora upande wa wanaume.

Jesca Lenga- Dodoma
Chipukizi (Kike)


Kutokana na kuwepo kwa tuzo ya mchezaji bora anayechipukia, ilishaeleweka wazi kuwa tuzo hiyo upande wa wanawake wa umri mdogo, ushindani mkubwa ulikuwa kwa mabinti wawili Jesca Lenga na Jesca Julius mmoja wapo ndiye angeshinda.


Uwezo wa wote wawili kwenye kufunga na kucheza kwa ubora wa hali ya juu ndio uliowapa nafasi kubwa ya kutabiriwa kushinda tuzo ya mchezaji bora kwa nyota wanaochipukia upande wa wanawake, na ndivyo ilivyokuwa.


Jesca Lenga wa timu ya wanawake mkoa wa Dodoma, alitangazwa mshindi wa tuzo hiyo na kuzawadiwa Sh200,000 na kumpoteza Jesca Julius wa CRDB.

Alex Clement -CRDB
Chipukizi Bora (Kiume)


Kifupi msimu uliopita CRDB ilikuwa na jambo lake pale Dodoma kwani, walionekana kupania na timu zao zilipambana hadi hatua ya nusu fainali.


Clement ndio alikuwa staa upande wa wachezaji chipukizi 'Best Rookie'. Moja ya mchezo uliokuwa wa kuvutia ni ule waliokutana na Dodoma ambao, ulimalizika kwa Dodoma kushinda kwa pointi 54-49.


Katika mchezo huo, Silyvian Yunzu wa Dodoma alimaliza kwa kufunga pointi 20, kati ya hizo alifunga katika maeneo ya mitupo mitatu mara nne na upande wa CRDB aliyebamba ni Clement aliyefunga pointi 14 na kuibuka mchezaji bora chipukizi.

Wengine waliotamba


Kwa upande wa Temeke aliyetamba alikuwa, Adinani Andrew alifunga pointi 15 na kufuatiwa na Fadhili Chuma (Mbeya) aliyefunga pointi 12, ambazo hazikufanikiwa kuibeba timu yake katika mchezo wa fainali.

Kwenye fainali ya wanawake, nyota Upendo Mpera wa Temeke ndio aling’ara akiongoza kwa kufunga pointi 16 huku akifutiwa na staa wao Rehema Silomba aliyefunga pointi 14.
Upande wa Dodoma Queens, aliyeng’ara ni Eveline Mihayo aliyefunga pointi 12 akifuatiwa na Jesca Lenga aliyefunga pointi 10.