MATAWINI: Huko Yanga mbona hawana presha

Muktasari:

  • TIMU gani inaongoza ligi? Ndio swali wanalouliza wanachama wa Yanga baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, na Namungo FC.

TIMU gani inaongoza ligi? Ndio swali wanalouliza wanachama wa Yanga baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, na Namungo FC.

Hayo yamesemwa na wanachama wa tawi la Yanga lililopo Chang’ombe Maduka Mawili kwa kile walichodai umoja waliokuwa nao utawafanya kutwaa ubingwa msimu huu licha ya kupata sare ya kwanza msimu huu.

Katibu Mkuu wa tawi hilo, Jaffar Salum alisema mateso waliyopitia miaka minne imekuwa fuzzo kwao kujirekebisha na kuja kivingine msimu huu.

“Timu inacheza vizuri sana ina wachezaji wenye kiwango kikubwa na kitu ambacho naamini kitatupa ubingwa ni ushindani wa namba uliopo kwani kila mchezaji anataka kumuonyesha kocha uwezo wake, hali ambayo kwa misimu iliyopita hakikuwepo,” alisema.

Kauli ya katibu huyo iliungwa mkono na Mwenyekiti msaidizi wa tawi hilo Athuman Onja akisema kinachowapa jeuri ya kutwaa ubingwa msimu huu ni matokeo mazuri wanayoendelea kuyapata.

“Pole pole ndio mwendo hiyo ndio kauli ambayo tunaitumia kwa sasa, ukiwaangalia wapinzani wetu wameanza kuwa na kiwewe mara tunanunua mechi na kadhalika lakini wanashindwa kutambua Yanga ya msimu huu ni bora zaidi yao,” alisema.

Naye mtunza fedha wa tawi hilo Abduswedy Juma alisema kuwa moja ya wachezaji wanaomvutia kwenye kikosi hicho ni pamoja na mshambuliaji Fiston Mayele kutokana na kujituma kwake kufunga mabao.

“Kikosi chote kimekamilika na kila mchezaji ananipa raha lakini kama unavyojua siku zote mfungaji ndiye anaonekana zaidi kuliko wengine,” alisema.

Mjumbe wa tawi hilo Jaffar Shaban alisema timu hiyo imekamilika kuanzia eneo la kipa mpaka ushambuliaji kitendo ambacho kinawatofautisha na timu nyingine.

“Ligi ya msimu huu Yanga peke yake ndiyo timu iliyokamilika tofauti na wengine ambao wamekuwa wakilaumiana tu kila kukicha,” alisema.

Tawi hili linaitwa Yanga Chang’ombe Maduka mawili, lilianzishwa Mwaka 1999, lina wanachama 1919, viongozi ni Mwenyekiti Mussa Ngwirizi, msaidizi wake ni Athuman Onja, Katibu Mkuu ni Jaffar Salum, msaidizi wake ni Tatu Leso, Mtunza fedha ni Abduswedy Juma.