Mayele apewa kazi ya TP Mazembe

Dar es Salaam. Kikosi cha Yanga kipo Lubumbashi, DR Congo kucheza mechi ya mwisho ya KUndi D ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe, wakati Fiston Mayele akicheza na mafaili ya miamba hiyo.

Wakati baadhi ya wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki wa Yanga wakitokea Tanzania kwenda Lubumbashi kuikabili Mazembe, Mayele alikuwa kwenye ndege nyingine kutoka Mauritania alikokuwa na timu yake ya taifa, DR Congo baada ya kumalizika kwa mechi ya kuwania kufuzu Afcon 2023 iliyoisha kwa sare ya 1-1, mchezo ambao Mayele aliingia akitokea benchi dakika ya 58 akichukua nafasi ya Aldo Kalulu.

Yanga imepania kushinda mchezo huo kwa mabao mengi ili kutinga robo fainali ikiongoza kundi hilo, jambo lililowafanya kutumia mbinu tofauti kuwasoma wapinzani hao na ili kuhakikisha jambo hilo linatimia, Mayele alitumiwa ‘video clip’ za mabeki na viungo wa Mazembe ili kuwasoma na kujua wanachezaji kabla ya kukutana, video alizozitazama wakati wote akiwa kwenye ndege kurejea DR Congo.

Yanga haina mpango wa kubadili kikosi, tofauti na kipa Djigui Diarra na kiungo Kharid Aucho wenye kadi za njano, hivyo Mayele mwenye mabao matatu hadi sasa katika hatua ya makundi ataendelea kuongoza safu ya ushambuliaji, Jumapili.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayele aliweka wazi kiu yake ya kuifunga Mazembe nyumbani baada ya kuwakosa Uwanja wa Mkapa katika mechi iliyomalizika kwa Yanga kushinda 3-1, mabao ya Keneddy Musonda, Mudathir Yahya na Tuisila Kisinda, huku akifafanua namna alivyojiandaa kutimiza hilo.

“Nimekutana na Mazembe mara kadhaa nikiwa AS Vita na sasa Yanga, huwa ni wapinzani wagumu, lakini natamani kuwafunga na kuisaidia timu kushinda mechi hii.

“Pamoja na kwamba wachezaji wengi wa Mazembe tunafahamiana, lakini nimejitahidi kuwafuatilia kwa karibu kujua wanachezaje.

“Kuna baadhi ya video zao nimepewa na viongozi wangu, naziangalia mara kwa mara kuhakikisha nawasoma vyema na najua aina yao ya kucheza ili kama nikipata nafasi nisisumbuke kufunga,” alisema.

Droo ya robo fainali inatarajiwa kuchezeshwa Jumatano, jijini Cairo, Misri, na mechi za kwanza zinatarajiwa kuchezwa kati ya Aprili 21 na 22, huku marudiano yakiwa kati ya April 28 na 29.