Mayele kama Garrincha na Diego Maradona

Garrincha wa Brazil

Katika historia ya Kombe la Dunia, ni wachezaji wawili tu wamewahi kuzibeba timu zao mabegani na kuzipata Kombe la Dunia.

Wachezaji hao ni Garrincha wa Brazil kwenye Kombe la Dunia la 1962 nchini Chile, na Maradona wa Argentina kwenye Kombe la Dunia la 1986 nchini Mexico.
Katika mafanikio ya timu zao, wachezaji hawa walitoa mchango zaidi ya nusu, na sehemu iliyobaki ndiyo iligawanywa na wenzao.

Magoli yao, pasi zao, maarifa yao, jitihada zao na hata majina yao, hivi vyote vilichangia sana kurahisisha mambo kwa timu zao.
 

Garrincha1962

Brazil ilienda Chile 1962 kama mabingwa watetezi wakiongozwa na Pele, nyota aliyeng'aa Sweden 1958 hadi kuchukua ubingwa.

Wakashinda 2-0 mchezo wa kwanza dhidi ya Mexico lakini katika mchezo wa pili dhidi ya Czechoslovakia, Pele akaumia na kushindwa kuendelea na mashindano.
Mchezo huo ukaisha kwa sare ya 0-0 iliyowaweka Brazil matatizoni, huku wakimpoteza shujaa wao.

Ndipo Garrincha aliposimama na kuibeba Brazil mgongoni kwake.
Alianzia kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Hispania ambao Brazil ilithitaji ushindi ili ifuzu.

Nafasi ya Pele ikachukuliwa na Amarildo, aliyefunga mabao mawili yaliyoipa Brazil ushindi wa 2-1.

Lakini mabao haya ni kama yalifungwa na Garrincha huku Amarildo akiwa amesaidia kuiweka tu mpira kwenye nyavu.

Garrincha alichukua mpira kutoka nje kidogo ya 18 yao, akapiga chenga wachezaji zaidi ya 6 na kumpa mfungaji amalizie.

Brazil ikafuzu kwa robo fainali na mpinzani akawa England.
Garrincha akaibeba tena mgongoni mwake Brazil, alifunga mabao mawili na kutengeneza moja kwa Vava. Brazil wakatinga nusu fainali na kukutana na wenyeji, Chile.
Garrincha akaibeba tena Brazil, akifunga mabao mawili na kusaidia moja, lililofungwa na Vava kwa mara nyingine.

Brazil wakatinga fainali na kukutana na Czechoslovakia, timu waliyokutana nayo hatua ya makundi hadi Pele kuumia.

Brazil ikashinda mchezo huu 3-1 na kutetea Kombe la Dunia huku Garrincha akiwa mfungaji bora na mchezaji bora wa mashindano.
 

Maradona 1986

Miaka 24 baada ya Garrincha, Maradona akarudia kazi yake, kwenye Kombe la Dunia 1986 nchini Mexico.

Maradona alienda kwenye mashindano haya akiwa amekaa nje ya soka la kimataifa tangu 1982 baada ya Kombe la Dunia.
Alipitia vipindi vingi mchanganyiko hapo kati, aliugua homa ya maini, kuzuiwa na klabu yake ya Napoli kurudi Argentina kuitumikia timu ya taifa na wakati mwingine ugumu wa usafiri.

Lakini alippofika Mexico akafidia muda wote huo. Huko ndiko alikofunga bao bora la muda wote la Kombe la Dunia, dhidi ya England.

Huko ndiko alikofunga bao maarufu na mkono wa Mungu, dhidi ya England. Huko ndiko alikofunga bao la maajabu dhidi ya Ubelgiji.

Maradona kama Garrincha, alifunga mabao mawili kwenye robo fainali, mawili kwenye nusu fainali na kuisaidia Argentina kuwa mabingwa.
Argentina wakawa mabingwa na Maradona akawa mchezaji bora wa mashindano.
 

Mayele 2022/23

Hakika msimu wa 2022/23 imekuwa wa maajabu sana kwa Yanga.
Baada ya kuondoshwa kwenye ligi ya mabingwa katika raundi ya pili na kuanza kwa kipigo cha 2-0 dhidi ya Monastir kwenye hatua ya makundi, Mayele akasimama imara kuibeba timu yake.

Kwenye mchezo wa pili dhidi ya TP Mazembe, Yanga walianza kwa kuongoza 2-0 kabla ya TP Mazembe kuja juu na kufunga moja kipindi cha pili.
Wakaukamata mchezo kiasi cha majukwaa yote ya mashabiki wa Yanga kuingia hofu na kuwa kimya.

Ally Kamwe, Afisa Habari wa Yanga, alisema.baada ya mchezo huu kwamba mashabiki walishakubali kushindwa huku walikaa kimya kusubiri Mazembe 'watufunge'.
Wakati mashabiki wakikubali kufungwa na Mazembe, Mayele hakukubali. Aliupokea mpira kutoka kwa Zawadi Mauya na kuanzisha shambulizi la kushtukiza kwa kasi ya ajabu sana.

Akaingia na mpira hadi eneo la hatari na kumpasia Tuisila Kisinda aliyefunga kwa shuti kali.

Yanga wakaenda ugenini nchini Mali kucheza na Stade Malien, na Mayele akafunga bao la maajabu kwa mguu ambao haujazoeleka, tena katika namna ngumu alivyosimama.

Wamali hao wakaja kwa Mkapa na Mayele akafunga tena bao moja katika mawili ya timu yake. Wakaja Monastir nao kukutana na kipigo cha 2-0 huku Mayele alifunga bao moja.
Yanga wakaingia robo fainali na kukutana na Rivers United ya Nigeria, walianzia ugenini.

Mayele akafunga mabao mawili muhimu yaliyorahisisha safari ya nusu fainali, licha ya suluhu ya nyumbani. Kwenye nusu fainali wakaja Marumo Gallants kutoka Afrika Kusini.

Mayele akawakosa Dar Es Salaam lakini akawakamatia kwao, bao moja la juhudi binafsi na pasi moja ya bao iliyotokana na juhudi binafsi pia, vilitosha kuwafikisha Yanga fainali.

Mchango wa Mayele hadi hapo ukawa tayari kama wa Maradona na Garrincha kwenye Kombe la Dunia.

Ni kweli kwamba timu nzima ya Yanga ilikuwa kwenye kiwango bora lakini Mayele alikuwa katikati ya ubora huo.

Bao la pili dhidi ya Marumo Gallants lililofungwa na Kennedy Musonda ni moja ya vipimo vinavyotoa majibu ya ubora wa Mayele.

Musonda aliingiza mpira wavuni lakini Mayele ndiye aliyefunga lile bao.
Mayele anastahili kuwa mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, hata kama Yanga hawatokuwa mabingwa mbele ya USM Alger.