Mayweather atawala pambano la mwisho kwake

Mayweather atawala pambano la mwisho kwake

Muktasari:

  • Kama ilivyobashiriwa, Floyd Mayweather alitawala pambano la kirafiki la raundi nane dhidi ya nyota wa YouTube, Logan Paul jana jijini Miami kabla ya kusema kuwa huo unaweza kuwa mchezo wake wa mwisho wa ngumi.

Miami, Marekani. Kama ilivyobashiriwa, Floyd Mayweather alitawala pambano la kirafiki la raundi nane dhidi ya nyota wa YouTube, Logan Paul jana jijini Miami kabla ya kusema kuwa huo unaweza kuwa mchezo wake wa mwisho wa ngumi.

Mayweather, ambaye alikuwa na uzito wa 155 lbs huku mpinzani wake akiwa na 189.5 lbs, alionyesha mchezo mzuri wenye ufanisi na kufurahisha mashabiki waliojazana uwanja wa Hard Rock katika jimbo la Florida.

Vipindi vya mara kwa mara vya mvua havikuweza kumzuia bondia huyo mwenye miaka 44 katika pambano lake la kwanza tangu Desemba mwaka 2018 alipomshinda mpinzani wake kutoka Japan anayecheza kick-boxing, Tenshin Nasukawa.

Huku watu kama bingwa wa zamani wa uzito wa juu duniani, Evander Holyfield akiwa jukwaani, Paul, mwenye miaka 26 alidumu kwa raundi zote nane za pambano hilo dhidi ya Mayweather, ambaye kwa nadra alitoka jasho.

Pambano hilo lilitangazwa kuwa la kirafiki badala ya lililopewa leseni, kitu ambacho kilimaanisha, hakukuw ana majaji na njia pekee ya kupata ushindi ilikuwa ni kusimamisha pambano au kushinda kwa knock-out ndani ya raundi nane zilizokuwa za dakika tatu kila moja.

Mayweather alistaafu ngumi mwaka 2017 akiw ana rekodi ya kushinda mapambano 50 bila ya kupoteza hata moja baada ya kumshinda bingwa aliyekuwa akitambuliwa na UFC, Conor McGregor jijini Las Vegas.

Paul, ambaye alikuwa akishiriki kwa mara ya tatu baada ya mapambano mawili ya kwanza dhidi ya nyota wenzake wa YouTube, alifunikwa na Mayweather ambaye alimsukumia makonde kadhaa, akimzuia kumsogelea.

Baadaye, Mayweather alidai kuwa pambano hilo linaweza kuwa la mwisho kwake, akisema "nilitaka kuwapa watu onyesho na (mpinzani wake) alikuwa akipambana kuokoa maisha.

"Hii ilikuwa akama mazoezi, hasa. Kwenda mbali kwake ilikuwa ni ushindi. Anaweza kukusogelea na alikuwa mzuri katika kukumbatia. Wakati mtu wa umbile lile anapokukumbatia, ni vigumu kumuondoa. Kama wanafurahia kushikana kwa raundi zote nane, basi ni vizuri kwao," alisema.

"Nilikuwana burudani. Ni vizuri. Wakati fedha zitakapokuja, tutaona nani ni mshindi.
"Nitarejea (jukwaani)? Bila shaka, hapana. Nimestaafu mchezo wa ngumi. Labda sitacheza pambano la kirafiki tena."