Mbrazil aanza na Chama, Luis mazoezini

Monday January 25 2021
mbrazili pic
By Thobias Sebastian

Straika Mnigeria, Junior Lokosa tayari ameshatua Dar es Salaam huku Kocha wa Makipa Mbrazili, Milton Nienov akiliamsha rasmi leo mazoezini.

Mastaa wa Simba waliingia kambini jana akiwemo Luis Jose na Clatous Chama na wote watakuwepo kwenye tizi la leo kujiandaa mechi za Simba Super Cup na mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Milton amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuwanoa makipa watatu wa Aishi Manula, Benno Kakolanya na Ally Salim na kulingana na uzoefu wake Afrika, Simba wamempa jukumu la kuanza mazoezi akimsubiri bosi wake atakayetambulishwa leo, Jijini Dar es Salaam.

Rekodi zinaonyesha miongoni mwa klabu kubwa alizowahi kuwa kocha, ni Vasco da Gama ya Brazil, FS Stars, Polokwane City na Golden Arrows za Sauzi.


MNIGERIA ATUA NA MIKWARA

Advertisement

Mchana wa jana Jumamosi saa 7:45 Junior Lokosa aliwasili nchini mara baada ya kumalizana na klabu yake ya zamani, Esperance Sportive de Tunis.

Lokosa alipokelewa na mkuu wa idara ya uendeshaji, Arnold Kashembe na habari zilizopatikana jana, ameanguka miezi sita kwanza kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Staa huyo aliliambia Mwanaspoti jana; “Ninao uzoefu wa kucheza mashindano haya makubwa lakini hata kucheza klabu kubwa kama Esperance Sportive de Tunis naimani hilo nitakuja kuliongeza katika timu hii ili kufanya vizuri.”

“Nimekuwa nikifanya vizuri katika kufunga katika timu mbalimbali nilizopita, najiamini katika kutekeleza jukumu langu hilo la kufunga naimani na hata hapa Simba nitakuwa na muendelezo wa kulitimiza hilo.

“Ndio kwanza nimefika hapa nchini siwezi kusema mambo mengi ila muda ambao nitakuwepo hapa na mechi nitakazocheza kila kitu tutaona,” alisema mchezaji huyo ambaye akiwa na Esperance Sportive de Tunis msimu wa 2019-20, alicheza mechi 11 na kufunga mabao mawili.

Rekodi za mtandaoni zinaonyesha amezaliwa Agosti 23, 1993, amecheza First Banka, Kano Pillars za Nigeria na Esperance. Ametumika pia katika timu ya taifa ya Nigeria mwaka 2018.

Advertisement