Mechi hii imebeba hatima ya Simba  

Muktasari:

  • Simba yenye pointi tano katika nafasi ya pili la kundi B ambalo linaongozwa na Asec yenye kumi na imeshafuzu, kimahesabu inahitaji ushindi kwenye mchezo wa leo saa 4:00 usiku.

Dar es Salaam. Hesabu za benchi la ufundi la Simba huko Ivory Coast leo, Ijumaa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ni kufanya kama ilivyokuwa kwa Horoya ya Guinea kwenye Uwanja wa Charles Konan (Yamoussoukro) ambapo mashabiki wa soka nchini humo walishindwa kuamini kilichotokea.

Nini kilitokea? Msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ASEC Mimosas ikiwa na matumaini ya kutinga hatua ya makundi, ilipigwa na kitu kizito katika raundi ya pili, mbele ya mashabiki wao baada ya kufungwa bao 1-0, ikiwa nyumbani dhidi ya Horoya na safari yao kwenye michuano hiyo mikubwa iliishia hapo maana kwenye mchezo wa awali huko Guinea ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Simba yenye pointi tano katika nafasi ya pili la kundi B ambalo linaongozwa na Asec yenye kumi na imeshafuzu, kimahesabu inahitaji ushindi kwenye mchezo wa leo saa 4:00 usiku, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny huko Abidjan ili kuweka hai matumaini ya kwenda robo fainali.

Rekodi zinaonyesha kwenye michezo 10 iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba imecheza ugenini, imeshinda mara nne dhidi ya Galaxy (2-0), Nyasa Big Bullets (2-0), 1º de Agosto (3-1) na Vipers (1-0), imetoa sare mbili dhidi ya Power Dynamos (2-2) na Galaxy (0-0).

Simba pia ilipoteza mara nne dhidi ya vigogo, Raja Casablanca (3-1), Wydad Casablanca mara mbili kila mchezo ilifungwa 1-0 na Horoya (1-0). Kwa takwimu hizo, Simba ina uwezo wa zaidi asilimia 50 wa kupata ushindi kwenye mchezo huu kutokana na mwenendo mzuri chini ya kocha Abdelhak Benchikha, na pia kutokana na rekodi yake nzuri kwenye michuano ya Afrika.

Akizungumzia mchezo huo na maandalizi ya mwisho ambayo Simba iliyafanya kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi (Stade de l’Ecole de Police) na wachezaji 22 waliosafiri, kocha mkuu, Benchikha alisema wapo tayari kwa mchezo huo ambao anatarajia kwamba utakuwa na ushindani wa aina yake.

"Tunatakiwa kucheza kwenye kiwango chetu bila ya kujali kwamba tupo ugenini, mpango wetu ni ushindi kwa sababu hayo ndio yatatuweka kwenye nafasi nzuri, tumekuwa na wakati mzuri kama timu kujiandaa kimchezo," alisema.  

Kwa upande wake, kipa wa Simba, Aishi Manula ambaye anatarajiwa kuanza kwenye mchezo huo kufuatia Ayoub Lakred kutumikia adhabu ya kadi, alisema pamoja na ugumu na umuhimu wa mchezo huo hawataingia kwa presha ili kufanikisha mpango wao.

"Hatutaogopa wala kuhofia bali tutafuata maelekezo ya walimu na lengo letu ni kuhakikisha tunashinda. Simba ni timu kubwa na tumecheza mechi nyingi za aina hii katika mazingira tofauti kwa hiyo tupo tayari kukabiliana na kila kitakachotokea," alisema kipa huyo mzoefu.

Katika mchezo wa mwisho wa Simba kucheza kwenye ligi dhidi ya JKT Tanzania, Benchikha alionekana kujaribu kutumia viungo watatu wote wenye asili ya kukaba japo mmoja ambaye alikuwa ni Sadio Kanoute alimpa uhuru wa kushambulia.

Fabrice Ngoma na Babacar Sarr, walicheza nyuma ya Kanoute huku Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza na Kibu Denis wakiwa sehemu ya safu ya ushambuliaji na licha ya changamoto ya ubora wa Uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo ufanisi wa wachezaji hao ulionekana  hivyo huenda Benchikha akaanza na nyota hao.

Shughuli inaweza kuwa pevu katika eneo la kati la uwanja kutokana na Asec Mimosas nao kuwa na wachezaji wenye ubora wa aina yake kama vile, Salifou Diarrassouba, Christian Kouame Koffi na Essis Baudelaire Aka ambaye ndiye nahodha wao kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Julien Chevalier.

Hata hivyo, wakati Simba ikimkosa Willy Esomba Onana aliyefanya vizuri kwenye michezo kadhaa ya michuano hiyo, ambaye anasumbuliwa na majeraha, Asec itacheza mara ya kwanza msimu huu bila staa wao mwenye mabao saba, Sankara Karamoko aliyeuzwa kwenye dirisha dogo.

Kimahesabu Simba ikishinda mchezo huu itafikisha pointi nane na kutafuta sare tu dhidi ya Jwaneng Galaxy kwenye mchezo wa mwisho nyumbani.

Mwamuzi
Refa Lahlou Benbraham kutoka Algeria ndiye atakayeuamua mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwamuzi huyu ametoa kadi za njano 22 na nyekundu moja msimu huu ndani ya michezo mitano tu aliyochezesha kwenye ligi ya Algeria ambayo ni maarufu kama Ligue Professionnelle 1 lakini hapa nchini anakumbukwa kwa kuchezesha mchezo kati ya Yanga na TP Mazembe, mechi ambayo Yanga ilishinda 1-0.

Tano zilizopita
25.11.23: Simba 1-1 ASEC Mimosas
20.03.22: ASEC Mimosas 3-0 Simba
13.02.22: Simba 3-1 ASEC Mimosas
19.10.03: ASEC Mimosas 4-3 Simba
24.08.03: Simba 1-0 ASEC Mimosas