Mechi ya heshima, burudani

Mechi ya heshima, burudani

Muktasari:

  • Soma ndani kwa uchambuzi zaidi wa mechi ya watani. Tuko LIVE pia kwenye mitandao yetu yote ya kijamii kukupa uhondo.

KUNA watu wawili leo watakuwa na kazi ngumu zaidi ndani ya ardhi ya Dar es Salaam. Kocha Didier Gomes wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga.

Gomes analazimika kwa namna yoyote kuishinda mechi ya leo dhidi ya Yanga kulinda hadhi yake na Bingwa mtetezi lakini vilevile kuendelea kujenga ushawishi kwa mabosi zake haswa baada ya kuongezeka kwa Kocha Mrundi, Hitimana Thiery kwenye benchi.

Lakini Nabi ni kama anatembea kwenye mkaa baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo, ikiwemo kutolewa kwenye michuano ya kimataifa mapema. Wadadisi wa mambo wanadai asiposhinda leo kibarua chake kipo kwenye hatihati baada ya Yanga kumshusha nchini, Cedrick Kaze ambaye ni Kocha mzoefu na kipenzi cha tajiri.

Kuanzia saa 11 watakuwa kwenye hali ngumu ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya kuiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam, ni wazi Gomes sasa amebakiza kibarua cha kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga leo, ushindi ambao utaifanya timu yake kumaliza tambo za Yanga kuwafunga mara nyingi zaidi mwaka huu.

Lakini kama watapoteza, maana yake, Simba itakuwa imefungwa mechi tatu na Yanga ndani ya mwaka mmoja jambo ambalo linaweza kumuweka kocha huyo na benchi lake la ufundi katika presha kubwa.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Gomes, mwenzake Nabi ndio amekalia kuti kavu zaidi na ushindi dhidi ya Simba leo ndio jambo linaloweza kulinda ugali wake ndani ya Yanga.

Nabi anaingia katika mechi ya leo akiwa na deni kubwa mbele kwa Yanga akihitajika kuwafuta machozi ya kuondolewa mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kichapo cha jumla cha mabao 2-0 kutoka kwa Rivers United ya Nigeria kwenye hatua ya awali.

Kana kwamba haitoshi, Yanga bado wana kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa kuadhimisha tamasha lao la Wiki ya Mwananchi dhidi ya Zanaco, Agosti 29 ambao walifungwa mabao 2-1.

Ulinzi haujawahi kutokea

Mchezo huo wa leo unaweza kuingia katika historia ya mechi za Watani wa jadi ambazo zimewahi kuwa na ulinzi wa hali ya juu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Kwa mujibu wa Mratibu Mkuu wa mechi hiyo, Baraka Kizuguto, kutakuwa na takribani askari 300 kutoka Jeshi la Polisi watakaoungana na maofisa kutoka vyombo vingine.

“Suala la ulinzi na usalama tumejipanga vilivyo na kudhihirisha hilo, kutakuwa na askari polisi kama 300 hivi ambao wataimarisha ulinzi kwa kutumia mbwan na farasi lakini pia kutakuwa na maofisa wa idara ya usalama wa taifa, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, kikosi cha zimamoto na uokoaji pamoja na kikosi cha Suma-JKT ambao ndio walinzi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa,” alisema Kizuguto.

Usimamizi kiweledi

Ni mchezo ambao utakuwa na usimamizi wa nyota tano kwa kuzingatia muongozo wa FIFA kwani utasimamiwa na jumla ya maofisa 14 kutoka ndani na nje ya nchi

Refa wa kati atakuwa ni Ramadhan Kayoko atakayesaidiwa na Frank Komba na Soud Lila huku wa akiba akiwa ni Elly Sasii wote wa hapa Dar es Salaam huku kamishna wa mchezo akiwa Sarah Chao na Kizuguto akiwa mratibu mkuu

Mtathmini wa waamuzi atatoka Burundi ambaye ni Jean Claude Birumushahu, Ofisa wa Ulinzi ni Inspekta wa Polisi, Hashim Abdallah, Ofisa Protokali ni Irene Mpulule, Ofisa Masoko ni Aaron Nyanda, Ofisa Habari ni Clifford Ndimbo, Daktari ni Lisobine Kisongo wakati Jonathan Kassano na Harieth Gilla wakiwa ni waratibu wasaidizi wa mchezo namba moja na namba mbili.


Mechi ya kufunguka

Usajili uliofanywa na timu hizo mbili pamoja na uhitaji wa matokeo ya ushindi kwa kila upande, vinatoa taswira ya wazi kwamba mechi ya leo kila timu itaingia na mpango wa kushambulia mara kwa mara badala ya kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza

Staili ya kuwakabia Simba katika eneo lao na kuwashambulia kwa kasi ilionekana kuzaa matunda kwa Yanga katika idadi kubwa ya mechi walizokutana na hapana shaka wanaweza kujaribu kuanza nayo tena leo. Lakini Simba nayo bila shaka itaanza mchezo huo kwa kushambulia ili kujaribu kuwazuia Yanga kusogea eneo lao

Hawa watabeba lawama

Kikosi cha Simba kinaweza kuwa hivi, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Joash Onyango, Enock Ibanga ‘Varane’ Lwanga Taddeo, Pape Sakho, Sadio Kanoute ,Chris Mugalu, Rally Bwalya, na Kibu Denis.

Kwa Yanga kikosi chao kinaweza kuundwa na Djigui Diarra,Shaban Djuma, Shomary Kibwana, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Yannick Bangala, Ducapel Moloko, Khalid Aucho, Fiston Mayele, Feisal Salum na Heritier Makambo.

Rekodi, historia vyachochea vita

Historia ya mechi za ngao ya jamii na rekodi ya nyuma ya timu hizo hapana shaka vitafanya mechi hiyo ya leo kuwa na ushindani na mvuto wa kipekee.

Katika mechi 10 zilizopita baina ya timu hizo, Simba imeibuka na ushindi mara nyingi ikifanya hivyo mara nne, Yanga imepata ushindi katika mechi tatu na michezo mingine mitatu zimetoka sare. Simba imefunga mabao tisa huku Yanga ikipachika mabao sita.

Tangu mwaka 2001 hadi sasa, Simba ndio kinara wa kutwaa Ngao ya Jamii ambapo wametwaa taji hilo mara tisa huku Yanga wakifuatia kwa kutwaa mara tano huku Mtibwa Sugar na Azam zikitwaa mara moja kila timu.

Katika mechi za mashindano tofauti na Ligi Kuu, timu hizo zimekutana mara 28 ambapo Simba wamepata ushindi mara 14, Yanga wameshinda mara 11 na sare tatu.

Katika mwaka huu, hadi sasa timu hizo zimekutana mara nne ambapo Yanga imeibuka na ushindi mara mbili, Simba mara moja na wakitoka sare katika mchezo mmoja.


Makocha wafunguka

Kocha Nabi alisema; “Hii sio tu mechi ya watani wa jadi bali pia ni taji na mshindi ni lazima apatikane na hii ni mechi inayofungua ligi na watu wengi wanaisubiria. Kwenye maandalizi tumefanya vizuri.

Siwezi mweledi hawezi kuahidi ushindi bali nitafanya kazi vizuri na benchi langu. Tumetolewa kimataifa hivyo mechi na Simba tunahitaji ushindi ili wachezaji, viongozi na mashabiki wawe na furaha,” alisema Nabi.

Nabi alisema katika mchezo huo atawakosa Mapinduzi Balama na Yassin Mustafa ambao bado hawajawa fiti baada ya kupona majeraha ya muda mrefu.

Kocha Didier Gomes amesisitiza kuwa mechi hiyo itakuwa ni ya kuvutia na yenye ufundi mkubwa kwani wamejiandaa vya kutosha huku akiwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwapa sapoti na kupata burudani.

Soma ndani kwa uchambuzi zaidi wa mechi ya watani. Tuko LIVE pia kwenye mitandao yetu yote ya kijamii kukupa uhondo.