Mfaransa ashtukia jambo sare ya Yanga

HUKO Jangwani mambo hayajatulia, kwani kuna maumivu flani yanayowapasua kichwa mabosi wa klabu hiyo na ghafla saa chache baada ya kuishuhudia timu yao ikilazimishwa sare nyingine katika Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, na kumuibua upya Mfaransa Sebastien Migne.

Mabosi wa juu wa Yanga walijifungia jana jijini Dar es Salaam katika kikao kizito wakijadili ujio wa kocha wao mpya Mfaransa Sebastian Migne wanayetaka kumpa ajira klabuni hapo.

Yanga inahitaji Migne na wako hatua za mwisho kumalizana naye na kiwango cha soka walichoonyesha wachezaji wao katika mchezo wa juzi dhidi ya KMC, ndio kimewafanya vigogo hao kuangalia namna gani watamaliza dili hilo la Mfaransa huyo mwenye uzoefu na soka la Afrika.

Mwanaspoti linafahamu, Yanga ilitaka kumleta mapema Migne, lakini kocha huyo akaomba amalize kula na familia yake Sikukuu ya Pasaka na ilikuwa mpaka kufikia Aprili 8 angekuwa ameshamaliza.

Hata hivyo, sare ya KMC ikafufua dili hilo na kuona kuna ulazima wa haraka wa Migne kuja nchini kushirikiana na kocha wa sasa wa muda, Juma Mwambusi.

Mapema jana Mwanaspoti lilichati na Migne akiwa kwao Ufaransa na kusema hana shida kuja Yanga kwani kwa sasa kuna mambo madogo yanatakiwa yamalizwe na mabosi wa Jangwani.

“Kuna mambo madogo tu yamebakia ili kila kitu kikae sawa na hakuna tatizo kwangu kama kuna mambo hayo yatawekwa sawa naamini yanaweza kumalizika tu,” alisema Migne.


MASTAA WAGOMEA KAMBI

Juzi baada ya mchezo wao dhidi ya KMC kumalizika kiwango cha timu hiyo kiliwakera mabosi na waliposikia kwamba wachezaji wao wamepewa mapumziko wakawa wakali wakitaka warudishwe kambini lakini mastaa hapo wakagoma.

Wachezaji walishindwa kukubaliana na msimamo huo wakisema wanataka kwenda kuona familia zao baada ya kukaa zaidi ya wiki mbili kambini.

Ratiba hiyo ya mapumziko awali ilikuwa imepangwa na kocha wa timu hiyo pamoja na wachezaji lakini kiwango cha soka walichokionyesha dhidi ya KMC kilionekana kutowafurahisha mabosi wao.

Hata hivyo mpaka basi la timu hiyo linaondoka uwanjani hapo halikuwa na mchezaji hata mmmoja zaidi ya viongozi wa benchi la ufundi huku wachezaji kila mmoja akiondika kivyake.


MWAMBUSI ATULIZA MASHABIKI

Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi amewatuliza mashabiki wa Yanga baada ya sare ya juzi dhidi ya KMC, kwa kusema wanaenda kurekebisha makosa yao yaliyowafanya washindwe kutoka na ushindi kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo ambao Yanga ililazimika kuchomoa bao kipindi cha pili kupitia Yacouba Songne, Mwambusi alisemasare hiyo haikuwa tarajio lake kutokana na namna alivyoiandaa timu, lakini anaenda kufanyia kazi makosa yaliyowanyima ushindi ili kuwapa raha wanayanga.

“Niseme wazi, baadhi ya wachezaji hawakuwa katika kiwango nilichokitegemea, kwani tulianza tukiwa chini mno kipindi cha kwanza, kabla ya kurejea kwa kasi kipindi cha pili na ndani ya dakika moja tu tulirudisha bao. Tulitengeneza nafasi nyingi lakini tulishindwa kuzitumia vizuri, tunatakiwa tukipata nafasi tuzitumie na hilo naenda kulifanyia kazi na kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Mwambusi aliyepewa timu baada ya kutimuliwa kwa kocha Cedric Kaze kutoka Burundi saa chache baada ya kutoka sare ya 1-1 na Polisi Tanzania Machi 7.