Mgunda achekelea, aitaja Yanga

NYOTA wa Simba wamerejea mazoezini kwa siku mbili na leo watalihama jiji kwenda Tanga kwa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, huku kocha Juma Mgunda akizungumzia matokeo ya mechi yao na Polisi na kupasuka kwa Yanga mbele ya Ihefu yameamsha ari mpya ya ubingwa.
Simba ilishinda mabao 3-1 ugenini dhidi ya Polisi mechi iliyopigwa mjini Moshi, huku Yanga ikipasuka ugenini mbele ya Ihefu jijini Mbeya na Mgunda alisema matokeo hayo yameirudisha kikosi hicho katika mbio za ubingwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31, moja pungufu na ilizonazo Yanga na Azam zilizopo juu yake na Mgunda alisema malengo makubwa kwa timu hiyo ni kukomaa na michezo iliyopo mbele ili kupata ushindi mingi ili kupunguza umbali wa pointi dhidi ya vinara Yanga iliyodondosha pointi.
Alisema ukiangalia matokeo dhidi ya Mbeya City kuna baadhi hata mashabiki walikuwa wameiona Simba imeondoka kwenye mbio za ubingwa, ila kuifunga Polisi na kupoteza kwa Yanga kumebadilisha upepo na sasa wanajipanga kuhakikisha wanafanya kweli hasa katika duru la pili.
"Kutokana na mwenendo wa ligi ulivyo umbali wa pointi walizotuacha Yanga na Azam na hali ya morali kwa wachezaji itaongezeka na tutapambana zaidi kupata matokeo mazuri," alisema Mgunda na kuongeza;
"Tuna kazi kubwa ya kufanya pamoja na wachezaji, kwani ushindani wa ligi umekuwa mkubwa kila mechi imekuwa ngumu ila tunahitaji kushinda mfululizo kwani bila ya kufanya hivyo malengo ya kutwaa ubingwa hayataweza kutimia."
"Niwapongeze wachezaji wangu licha ya ugumu wa ratiba kucheza mechi kila baada ya siku tatu wamekuwa wakipambana na kuhakikisha Simba inapata matokeo mazuri kwani bila ya ubora wao kazi itakuwa ngumu kwa upande wangu. Nimekaa nao kuzungumza nao kila mmoja kufahamu tunatakiwa kupambana kadri ambavyo inawezekana kila mmoja kutimiza majukumu ili kufikia malengo."
Simba inaondoka leo kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Wagosi itakayopigwa Jumamosi, jijini Tanga, huku rekodi zikiwabeba mbele ya wenyeji wao kila wanapokuta iwe ugenini ama nyumbani.