Mgunda awashtua Simba, awavuruga wazungu

Mgunda akumbukia ya Jwaneng Galaxy kwa Simba

SIMBA sasa inachekelea kutinga hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuiondosha Nyassa Big Bullets ya Malawi kwa matokeo ya jumla ya 4-0 lakini kubwa zaidi ni rekodi na mwenendo bora wa kocha wa muda, Juma Mgunda ‘Guardiola Mnene’ vimewasapraizi wengi.

Mgunda alikabidhiwa kijiti cha kuinoa Simba kama kocha wa mpito, Septemba 7, 2022 siku chache kabla ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mserbia Zoran Maki aliyedumu kwa siku 70 ikiwa sawa na mwezi mmoja na siku 10 tu.

Kibarua cha kwanza kwa Mgunda kilikuwa kuisimamia Simba kwenye mechi ya kwanza ya mtoano Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Nyassa Big Bullets Malawi na akafanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 siku tatu tu baada ya kupewa timu, mabao yakifungwa na Moses Phiri na nahodha John Bocco.

Baada ya hapo Simba ilirejea Dar es Salaam kisha kusafiri hadi Mbeya kucheza mechi ya Ligi dhidi ya Tanzania Prisons timu ambayo imekuwa ngumu kwa Mnyama akishindwa kupata ushindi katika miaka mitatu ya hivi karibuni ugenini chini ya makocha tofauti lakini Mgunda akashinda.

Kwa mara ya mwisho Simba kupata ushindi ugenini dhidi ya Prisons ilikuwa msimu wa 2018/2019 chini ya kocha Mbelgiji Patrick Ausems ikishinda 1-0 na baada ya hapo haikushinda iliambulia suluhu moja tu msimu uliofuata (2019/20) chini ya Kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck lakini hakuepuka kichapo kwani msimu uliofuta 2020/21, alikubali kichapo cha bao 1-0 na msimu uliopita Simba ikiwa chini ya Seleman Matola ikachapwa 1-0 tena.

Mgunda alivunja mwiko huo, na mechi iliyofuata ilikuwa ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyassa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuiongoza kupata ushindi wa 2-0 mabao yote yakifungwa na Phiri na kutinga hatua ya kwanza ya michuano hiyo itakapokutana na Premiero de Agosto ya Angola.

Tangu ameichukua Simba, Mgunda ameiongoza kwenye mechi tatu za mashindano na kushinda zote kwa jumla ya mabao matano bila kuruhusu hata moja huku kikosi kikionekana kubadilika na ubora wa wachezaji kuongezeka pamoja na morali.

Kati ya vitu alivyoviboresha Mgunda ndani ya Simba hadi sasa ni kuwajengea uwezo na maelewano wachezaji mfano kumuingiza beki Kennedy Juma kikosini na kuziba pancha za kina Mohammed Ouattara na Henock Inonga katika eneo la beki ya kati kutokana na wawili hao kuonekana kuwa na sifa zinazofanana.

Kingine ni kumuanzisha kwa mara ya kwanza kikosini nyota Mghana Augustine Okrah kwenye mechi dhidi ya Nyassa kama winga wa kushoto na nyota huyo kuonyesha ubora wake ambao mashabiki wengi wa Simba waliusubiri kwa hamu.

Pamoja na hayo, Mgunda ana sababu nyingi za kuwafanya mabosi wa Simba kuendelea kumuamini na ikiwezekana kukabidhiwa timu kutokana na mechi zilizo mbele yake kuliko kuleta kocha mpya.

Katika kipindi hiki cha mapumziko ya mechi za timu za taifa, Mgunda atainoa Simba na kufundisha mifumo na mbinu zake jambo ambalo litaongeza ubora kikosini kuelekea mechi ijayo ya Ligi Septemba 28 dhidi ya Mbeya City ugenini.

Baada ya hapo Simba itaanza kucheza karata zake kimataifa ugenini Angola dhidi ya Agosto, ambayo imeimarika zaidi na baadaye kuwakaribisha nyumbani jambo ambalo kama viongozi wa timu hiyo wataamua kuleta kocha mpya wanaweza kuwavuruga tena wachezaji kutoka kwenye mbinu za Mgunda hadi za kocha mpya na ikumbukwe hakuna mapumziko hapo na mwezi huo huo watakuwa na mechi tena dhidi ya Yanga Oktoba 23.

Huenda ikawa ngumu kwa vingozi wa Simba kuamini katika kocha mzawa ‘Mgunda’ lakini katika uamuzi wao wanahitaji kurejea historia za makocha wazawa watano watakaoziongoza timu tano za Afrika kwenye Kombe la Dunia litakaloanza Novemba 20, 2022 nchini Qatar.

Makocha hao ni Walid Regragui wa Morroco, Aliou Cisse wa Senegal, Rigobert Song wa Cameroon, Otto Addo wa Ghana na Jalel Kadri wa Tunisia.