Mipango ya Simba fainali za Caf iko hivi

Muktasari:

KAMA kuna mtu anayedhani Simba imebahatisha kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, basi pole yake kwani mabosi wa klabu hiyo wamefichua kwamba kila jambo lilipangwa kabla ya msimu kuanza na hatua ijayo ni lazima watoboe hata kufika fainali ikiwezekana.

KAMA kuna mtu anayedhani Simba imebahatisha kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, basi pole yake kwani mabosi wa klabu hiyo wamefichua kwamba kila jambo lilipangwa kabla ya msimu kuanza na hatua ijayo ni lazima watoboe hata kufika fainali ikiwezekana.

Simba imeandika historia kwa timu za Tanzania kwa kumaliza kinara wa kundi kwa kushinda mechi nne, sare moja na kipigo kimoja ikikusanya pointi 13 mbele ya watetezi Al Ahly ya Misri na sasa inasubiri kujua itapangwa na nani katika robo fainali.

Wakisubiri kujua itacheza na MC Alger, CR Belouizdad ama Kaizer Chiefs, viongozi wa Simba wameendelea kusisitiza baada ya kutinga hatua hiyo kwa sasa wanaifikiria zaidi nusu fainali, kwani hawaoni kitakachowazuia. Droo ya hatua hiyo itapangwa Cairo Misri, Aprili 30.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu aliliambia Mwanaspoti mara baada ya kuwasili nchini na msafara wa timu huyo kutoka Cairo, Misri ilipoenda kucheza na Al Ahly na kulala 1-0 kuwa, kiu yao kwa sasa ni kufika nusu fainali, baada ya lengo lao la kwanza kufanikiwa.

“Tunawapongeza sana wachezaji na benchi la ufundi kwa namna ambavyo wamepambana kadri wawezavyo kupata matokeo haya waliyoyapata katika michezo ya makundi,” alisema Mangungu na kuongeza:

“Awali tulijiwekea lengo la kufika robo fainali, kwa vile tumefanikiwa sasa ni zamu ya kuitafuta nusu fainali na tukitoka hapo itakuwa ni fainali na ubingwa wa Afrika kwa ujumla, inawezekana kwa vile tulishajipanga mapema, watu wasidhani tumebahatisha kwa mafanikio haya.

“Uongozi unatimiza majukumu ili kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi linakuwa sawa muda wote na morali zao zikiwa juu zaidi, ili kufikia malengo hayo na tunaamini kwa umoja wetu tutafika Inshallah!” alisisitiza Mwenyekiti huyo aliyechaguliwa hivi karibuni kuziba nafasi ya Swedy Nkwabi.

Alisema kwa sasa baada ya kurejea nchini wanaanza maandalizi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC, ambapo ratiba inaonyesha kabla ya kuanza mechi zao za robo fainali kwa Afrika itacheza mechi nane za VPL ikiwamo pambano la watani wao, Yanga na mechi ya 16 Bora ya ASFC.

Imeandikwa na Clezencia Tryphone, Olipa Assa na Thobias Sebastian