Msafara wa Yanga, GSM, Tarimba ndani

Dar es Saalam. Katika kuonyesha kuwa Yanga inahitaji ushindi katika mchezo wao wa ugenini dhidi ya TP Mazembe msafara wao umewajumuisha watu wazito watano wa juu katika klabu hiyo.

Yanga ambayo inaondoka kesho asubuhi na ndege ya Shirika la Tanzania msafara wao utawajumuisha wajumbe wawili wa Baraza lao la Wadhamini Tarimba Abbas na Geofrey Mwambe.

Msafara huo utakaokuwa na jumla ya watu 44 pia atakuwemo mfadhili wa klabu hiyo Ghalib Said Mohamed na Rais wa Yanga injinia Hersi Said.

Yanga ambao ni vinara wa kundi lao D kwenye mechi za Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakilingana na US MONASTIR inajipanga kusaka ushindi katika mchezo huo  wa Jumapili Aprili 2 jijini Lubumbashi dhidi ya Mazembe kwa lengo la kutaka kusalia na kumaliza vinara kwenye kundi lao.

 Mazembe inayoshika mkia katika kundi lao haina nafasi yoyote ya kusonga mbele katika kundi hilo wakiwa na alama 3 huku juu yao wakiwa Real Bamako ya Mali wenye alama 5.
 
 Ushindi wa Wakongomani hao mbele ya Yanga  utakuwa na lengo la kulinda heshima yao pekee  ya kutomaliza mkiani huku wakiwaombea mabaya Bamako wapoteze ugenini dhidi ya Monastir mechi zote zikipigwa muda mmoja.