Mtemi amuuma sikio Gomes kwa Al Ahly

Muktasari:

  • Simba imeshauriwa kumaliza nyumbani mechi yao na Al Ahly huku kocha Didier Gomes akishauriwa kubadili mbinu za kiufundi katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CCL).

Dar es Salaam. Simba imeshauriwa kumaliza nyumbani mechi yao na Al Ahly huku kocha Didier Gomes akishauriwa kubadili mbinu za kiufundi katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CCL).

Simba itakuwa mwenyeji wa Al Ahly ya Misri Februari 23 katika mechi ya pili ya Kundi A, baada ya awali kuichapa AS Vita bao 1-0 ugenini nchini DR Congo baada ya mechi hiyo, itacheza na Al Merrikh ya Sudan kabla ya mechi za marudiano.

Mechi na Al Ahly ndiyo imetajwa na nyota huyo wa zamani, Mtemi Ramadhani kuwa ngumu zaidi kwa Simba katika hatua ya makundi, huku Gomes akishauriwa kubadili mfumo wa kuwa anamtumia mshambuliaji mmoja.

“Amekuwa akimtumia Mugalu (Chris) au Kagere (Meddie), pale mbele, lakini kwenye mechi na Al Ahly kumuanzisha mmoja pekee haitoshi,” alisema Mtemi.

Alisema kwa jinsi alivyowatazama kwenye mechi zao za hivi karibuni, ni tiu ambayo wachezaji wake wote wako fiti tofauti na Al Ahly iliyowahi kuja kucheza nchini miaka ya nyuma.

“Kwa hii Al Ahly ya sasa, Simba ifanye iwezavyo imalize mechi yao nyumbani, kule Misri binafsi naona kwa namna yoyote ile Simba tutafungwa,” alisema Mtemi.


Namungo kurejea, wanne wabaki

Kikosi cha Namungo kinarejea nchini kutoka Angola bila nyota wake watatu na kiongozi mmoja kutokana na kuzuiliwa nchini humo kwa madai ya kukutwa na ugonjwa wa corona.

Wachezaji walibaki ni Lucas Kikoti, Fred Tangalu na Khamis Faki sambamba na Mtendaji Mkuu Omary Kaaya, ambao walitengwa sehemu tofauti na wenzao.