Mukoko aitia pancha Yanga

KATIKA Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kunakopigwa mechi ya fainali ya kombe la Azam (ASFC) kati ya Simba na Yanga dakika 45 za kipindi cha kwanza zimemalizika kwa suluhu (0-0) huku yanga wakimaliza pungufu.

Yanga ndio walianzisha mpira kupitia kwa Yacouba Songne aliyeanza kwa kupiga pasi ndefu katika eneo la Simba mpira uliokimbiliwa na Kisinda na kuingia nao eneo la hatari lakini ukatoka nje.

Mechi hiyo ilianza kwa presha kubwa kwa timu zote mbili kila moja ikicheza kwa kujihami kwa dakika 15 za awali na baada ya hapo utulivubulianza kuonekana.

Mashabiki waliojaa uwanjani hapo kila mmoja akuwa upande wa chama lake walionekana kushangilia, kuzomea na kutamba kwa dakika zote 45.

Dakika ya 12 Clatous Chama wa Simba alioneshwa kadi ya njano baada ya kuonekana kumjibu kwa hasira mwamuzi wa kati wa mchezo huo wa leo.

Presha ya mechi iliendelea kuwa kubwa kwa wachezaji, waamuzi na mashabiki na dakika ya 25 mashabiki wa Simba walionekana wakimrushia chupa mwamuzi wa ziada ‘kibendera’ kwa kile walichoamini kuwa ametoa maamuzi yasiyosahihi kwa kuwapa Yanga faulo baada ya kutokea purukushani kati ya Tusila Kisinda na Mohamed Hussein.

Namna dakika zilivyozidi kwenda, Simba walikuwa wakionekana bora zaidi ya Yanga huku Simba hao hao wakimlalamikia refa mara kwa mara.

Dakika ya 45, mwamuzi wa mchezo huo, Ahmed Arajiga alimuonesha kadi nyekundu ya moja kwa moja kiungo wa Yanga, Mukoko Tonombe baada ya kumchezea faulo nahodha wa Simba John Bocco na Yanga kubaki pungufu uwanjani.

Pamoja na yote hayo, hadi dakika 45 za kioindi cha kwanza hakuna timu ambayo ilikuwa imepata bao.