Mukoko atema nyongo Yanga, aiba madini Simba

Mukoko atema nyongo Yanga, aiba madini Simba

Muktasari:

  • MASHABIKI wa Yanga bado hawana furaha na timu yao na wala hawakubaliani na jinsi chama lao linavyotaabika mbele ya timu ndogo katika mechi zao za Ligi Kuu Bara, lakini kiungo wao, Mukoko Tonombe naye ametia neno kwa mastaa wote akiwamo yeye kuwa wanastahili lawama hasa kama watashindwa kutimiza lengo la kubeba ubingwa.

MASHABIKI wa Yanga bado hawana furaha na timu yao na wala hawakubaliani na jinsi chama lao linavyotaabika mbele ya timu ndogo katika mechi zao za Ligi Kuu Bara, lakini kiungo wao, Mukoko Tonombe naye ametia neno kwa mastaa wote akiwamo yeye kuwa wanastahili lawama hasa kama watashindwa kutimiza lengo la kubeba ubingwa.

Juzi kati Yanga ilipata sare ya tisa, ikigawana pointi na KMC katika mechi kali ikiifanya timu hiyo kuzidi kuzidondosha pointi kupitia sare mbali na kipigo kimoja ilichopewa na Coastal Union mapema mwezi uliopita.

Sare hiyo imeifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi 21 ilizotema mpaka sasa msimu huu, na kutoa nafasi kwa wapinzani wao Simba na Azam waliokuwa wamewaacha mbali hapo awali kuwasogelea na kutishia mipango yao ya kurejesha taji Jangwani baada ya misimu mitatu mfululizo likiwa mikononi mwa Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti huku akionekana kuchukua Mukoko alisema hana uhakika kwamba kama ndoto zao za kuwa mabingwa msimu huu zitatimia kutokana na hatua ya kuendelea kudondosha pointi.

“Sioni uhakika wa hilo naona tunazidi kujiweka katika nafasi ngumu kwenye malengo hayo (ya ubingwa), sio hatua nzuri kuendelea kuangusha pointi,tulipaswa kuendelea kushinda lakini hali haiko hivyo,” alisema Mukoko na kuongeza;

“Matokeo yetu yanazidi kutupunguza nguvu lakini yanatoa morali kwa tunaofukuzana nao hapo ndio ugumu unakuja.”

Mukoko alisema endapo Yanga itakosa ubingwa basi wa kwanza kulaumiwa ni wao kama wachezaji kwa kushindwa kutimiza malengo ya klabu.

Kiungo huyo Mkongomani alisema bado kuna utofauti mkubwa wa madaraja ya wachezaji wenzake katika ubora hali ambayo imekuwa ikitoa nafasi kwa wapinzani kupata pointi katika mechi zao.

“Hatujaweza kucheza kwa ubora mkubwa tukiwa kama wachezaji wa Yanga, nawaonea huruma mashabiki na hata uongozi walitarajia makubwa lakini tumewaangusha,” alisema Mukoko na kuongeza;

“Sikuzote nimekuwa nikisema kwamba hii ni klabu kubwa unaposaini mkataba wa kuja hapa unatakiwa kuelewa unaingia katika klabu ambayo unatakiwa kupambana ishinde.”

SOKA LA SAIDO

Akiendelea kutoa mifano Mukoko alisema kuna kundi kubwa la wachezaji wenzake wanapaswa kujifunza kupitia ubora wa mkongwe wa timu hiyo Said Ntibazonkiza ‘Saido’ ambaye licha ya kuwa amecheza soka kwa mafanikio makubwa Ulaya lakini bado anapambana.

“Angalia Saido amecheza Ulaya kwa muda mrefu amepata mafanikio makubwa ambayo wengine ndio tunayaota kufika huko lakini bado anapambana. Soka ni mchezo ambao watu mnaweza kufanya makosa lakini hatua nzuri ni kila mchezaji anatakiwa aweze kujirekebisha,huwezi kufanikiwa kama unaona makosa yako ni sehemu ya mafanikio,” alisema Mukoko na kuongeza;

“Unapokuwa uwanjani unamuona jinsi anavyoipigania timu tulipaswa wachezaji wengi kujifunza hiki na kupambana vile huwezi kubwa bingwa kama hujaweza kupambana kwa kiwango kama kile.

AIBA MADINI MSIMBAZI

Aidha Mukoko aliendelea kutema nyongo akisema kipo kitu cha kujifunza kutoka kwa watani wao Simba ambao kikosi chao kina nyota wanne tu kwenye uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza huku wengine wakiwa wa kigeni lakini wenye ubora.

“Tunatakiwa kuwa bora angalia Simba wakicheza mechi kubwa yenye ushindani ni wachezaji watatu wenye ubora wa kuanza, kuna Manula(Aishi), beki wa kulia (Shomari Kapombe) na yule wa kushoto(Mohammed Hussein),” alisema Mukoko na kuongeza;

“Hao wataanza sio kwa vile ni wazawa, ila wanastahili kwa ubora wao na wengine 8 watakaocheza ni wa kigeni na wenye ubora hili linapaswa kuwa na hapa. Kama unashindwa kukaba au kufunga mazoezini huwezi kufanya hivyo katika mechi na hapa ndipo tunapata anguko.”