Mwakalebela apelekwa Kamati maalumu TFF

Mwakalebela apelekwa Kamati maalumu TFF

Muktasari:

  • BAADA ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kuzishutumu mamlaka zinazosimamia mpira wa miguu nchini kuwa haziitendei haki klabu yake, sasa shauri lake limepelekwa katika kamati maalumu kusikilizwa.

BAADA ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kuzishutumu mamlaka zinazosimamia mpira wa miguu nchini kuwa haziitendei haki klabu yake, sasa shauri lake limepelekwa katika kamati maalumu kusikilizwa.

Februari 19 mwaka huu, Mwakalebela alipozungumza na waandishi wa habari na katika maelezo yake alizishutumu mamlaka zinazosimamia soka kuwa haziitendei haki Yanga hususani katika suala la maamuzi ya viwanjani.

"Yanga tumeona kwamba hatutendewi haki na vyombo vinavyosimamia mpira kwa maana ya Shirikisho la Soka Tanzania 'TFF', Bodi ya Ligi na Kamati ya Saa 72 pamoja na kamati ya waamuzi," alinukuliwa Mwakalebela.

Baada ya shutuma hizo, Kamati ya Uendeshaji na usimamizi wa ligi na Bodi ya Ligi Kuu Bara katika kikao chake cha Februari 24, 2021 ilipitioa mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kufanya maamuzi ikiwemo pia suala hilo la Mwakalebela.
Taarifa iliyotolewa na bodi hiyo kupitia idara ya habari na mawasiliano jana Februari 25, bodi hiyo ilieleza hivi.

"Baada ya kupitia shutuma hizo (kuhusu Mwakalebela), kamati imeona kuna haja ya mtoa shutuma kupewa haki ya msingi ya kusikilizwa na kuthibitisha madai yake mbele ya kamati husika. kutokana na hilo, kamati inaliwakilisha suala hilo TFF kwa ajili ya kupelekwa kwenye kamati yenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo," imeeleza.

UONGOZI  YANGA WAFUNGUKA
Katibu wa Yanga Haji Mfikirwa ambaye pia alitangaza klabu hiyo kuonewa na vyombo vinavyosimamia mpira hapa nchini na kupelekea timu yao kutopata matokeo katika mchezo wao na Kagera Sugar na Mbeya City ambao waliambulia sare alisema hawana shida kiongozi wao kupelekwa TFF.

Mfikirwa amesema Mwakalebela ataenda huko anakoitwa ili kujieleza kwani malalamiko waliyoyatoa wana uhakika na ushahidi upo kwani mpira unachezwa wazi.

"Mpira unachezwa wazi, hauchezwi chumbani, video zipo hakuna shida, atatii wito na hatukusema kwa kukurupuka tulijiridhisha juu ya hilo,"amesema Mfikirwa.