Mwana FA ataka wadau kusaidia klabu Ligi Kuu
Naibu Waziri Wa Utamaduni, Sanaa Na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) amezitaka taasisi za fedha na kampuni za bima kuongeza ufadhili wao kwenye sekta ya michezo na burudani ili kuchochea zaidi kasi ya ukuaji wa sekta hiyo.
Mwinjuma ameyasema hayo kwenye msimu wa kwanza wa Tamasha la Bima Festival wakati akizindua ambapo aliwasihi wadau wajitokeze zaidi kuunga mkono shughuli mbalimbali zinazofanywa na wadau wa michezo na burudani nchini kwa kudhamini shughuli zao mbalimbali na kuwatumia kwenye hamasa za kibiashara yakiwemo matangazo.
“Mchango wenu unaweza kutafsiriwa katika maeneo mengi ya kimichezo lakini msisitizo wangu nauweka zaidi katika udhamini wa matukio mbalimbali ya michezo husani katika uibuaji wa vipaji na kusaidia klabu mbalimbali zinavyoshiriki ligi mbalimbali hapa nchini ikiwemo Ligi Kuu. Zaidi pia niwaombe muendelee kubuni huduma za bima na huduma za kifedha mahususi kwa wanamichezo na wasanii ili muwasaidie kulinda afya na kazi zao na zaidi kuwajenga kiuchumi,’’ alisema Mwinjuma
Katika tamasha hilo benki ya Exim ambao ndio waandaaji waliiibuka mshindi wa jumla kwenye mashindano ya mpira wa miguu yaliyohusisha wadau wote.
Mwinjuma aliipongeza benki hiyo kwa jitihada zake za kukuza michezo hapa nchini kupitia msaada wa vifaa vya michezo inavyotoa kwa shule za msingi na sekondari katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
"Mmeonyesha dhamira na nia njema ya kuinua vipaji vya vijana na kuwezesha maendeleo ya michezo nchini. Tunatambua mchango wenu mkubwa katika kuendeleza michezo na tunawashukuru kwa kuwa wabia wetu katika kufanikisha malengo yetu ya kitaifa katika sekta hii,” alisema Mwinjuma
Awali, akizungumza kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Exim, Mkuu wa Idara ya uwekezaji kimkakati na matawi ya nje, Sumit Shekhar, alisema kupitia tamasha hilo litakalokuwa likifanyika kila mwaka, wamejipanga kutumia vema fursa ya michezo na burudani kuboresha mahusiano yake na wadau wake mbalimbali wakiwemo wateja, wadau wa bima, wafanyakazi, mamlaka mbalimbali zinazosimamia sekta ya bima na benki pamoja na serikali.