Mwanadada fundi wa kuchezea mpira akutwa amefia ndani

Muktasari:
- Hadhara aliyejizolea umaarufu mkubwa enzi za uhai wake kwa kipaji cha kuuchezea mpira atakavyo, amekutwa amefariki dunia ndani akiwa peke yake.
Dar es Salaam. Fundi wa kuchezea mpira, Hadhara Charles amefariki dunia baada ya mwili wake kukutwa ndani kwake akidaiwa kufariki tangu siku tatu zilizopita.
Mwili wa mwanadada huyo ulilazimika kuzikwa jana usiku Juni 11, 2025 katika makazi yake aliyokuwa akiishi eneo la Chanika jijini Dar es Salaam.
Hadhara aliyejizolea umaarufu mkubwa enzi za uhai wake kwa kipaji cha kuuchezea mpira atakavyo, ambapo wengi walipenda kumuita Gaucho.
Mdogo wa Hadhara aliyejitambulisha kwa jina la Mama Raiyan ameieleza Mwananchi namna kifo cha dada yake kilivyotokea na kwa jinsi mwili ulivyoharibika mazishi yake yatafanyika kwa haraka.
"Hadhara alikuwa na changamoto ya kifafa ambacho kadri muda unavyokwenda ndivyo kilikuwa kinazidi, Chanika alikojenga alikuwa anaishi peke yake na majirani wamesikia harafu ndipo wakajua amefariki," amesema mdogo wake huyo na kuongeza;
"Kwa namna alivyoharibika anazikwa leo leo (jana usiku) hapo hapo nyumbani kwake, kama ni kifo kitakuwa kimemtokea Jumapili, maana sikukuu ya juzi tumekula naye nyumbani.
"Ndugu waliopo maeneo jirani kama Mbagala hao ndiyo watabahatika kuzika, mimi mwenyewe nipo Tegeta nina watoto wawili wadogo nimeshindwa kuwahi kwa jinsi inavyoelezwa mwili umeharibika vibaya, baada ya kumpumzisha ndipo tutajua kipi kitaendelea."
Katika mahojiano aliyowahi kufanya na Mwananchi alieleza namna ugonjwa uliokuwa unamsumbua unavompa misukosuko katika maisha yake.
"Nasumbuliwa sana na ugonjwa wa kifafa, kuna wakati nilikuwa nikisafiri kwenda nje kwenye shoo changamoto hiyo ilikuwa inanikumba, msaada wangu ilikuwa ni wale ambao naongozana nao," alisema.
Enzi za uhai wake, Hadhara licha ya video zake kusambaa mitandaoni kuytokana na ufundi wake wa kuchezea mpira kuanzia hata kwa miguu aliwahi kusifiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump kutokana na video yake iliyochapishwa mitandaoni.