Nabi: Acheni waje, awachorea ramani mapema

Muktasari:

  • KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, huku kocha Nasreddine Nabi akisema hana presha na wapinzani wao, lakini akili yake ipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akitaka kuifika hatua ya makundi, huku akikiri mtego huo kwa Waarabu.

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, huku kocha Nasreddine Nabi akisema hana presha na wapinzani wao, lakini akili yake ipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akitaka kuifika hatua ya makundi, huku akikiri mtego huo kwa Waarabu.

Nabi ameiangalia ratiba ya CAF iliyotolewa juzi na kuichambua kwa utulivu akisema anataka kwanza kumalizana na watani wao, Simba watakaocheza nao Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kisha kushughulika na wapinzani wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ratiba iliyotoka juzi mchana inaonyesha Yanga itaanza na Zalan FC ya Sudan Kusini na mabingwa hao wa Tanzania wataanzia ugenini kisha kumalizia nyumbani na kama itapenya hapo itavaana na mshindi kati ya St George ya Ethiopia au matajiri Al Hilal ya Sudan.

Akizungumzia ratiba hiyo, Nabi alisema timu yake siyo kwamba itakuwa na wepesi kutokana na ubora tofauti wa wapinzani wao.

Hata hivyo, alisema Yanga haitaweza kutolewa kirahisi na Zalan kutokana na ubora wa kikosi chake ingawa hawatakiwi kuwadharau.

“Sio timu kubwa (Zalan), lakini hatutakiwi kuwadharau hata kidogo. Tunatakiwa kutambua wamemaliza sehemu ambayo wanahitaji kuheshimiwa mpaka wanacheza hatua hii ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Nabi ambaye juzi Agosti 9 alitimiza umri wa miaka 57 ya kuzaliwa.

“Tuna timu kubwa kuliko wao, lakini ukubwa wetu tunatakiwa kwenda kuuthibitisha katika dakika 180 dhidi yao katika mechi hizo mbili tutakazokutana nazo.”

Nabi aliongeza kuwa pasua kichwa ni nani watakutana naye kama watafuzu hatua hiyo, lakini akasema timu ngumu kwao itakuwa ni Al Hilal ambayo inafundishwa na kocha Mkongomani Florent Ibenge aliyechukua Kombe la Shirikisho akiwa na RS Berkane ya Morocco msimu uliopita.

Alisema Al Hilal ni timu ambayo msimu ujao itakuwa na tofauti kutokana na aina ya usajili mkubwa ambao wameufanya msimu huu, ingawa Yanga haitakiwi kuwaogopa zaidi, bali kujipanga.

Al Hilal msimu huu iliwatingisha Yanga ikitaka kumchukua mfungaji wao bora Fiston Mayele ambapo walipomkosa Mkongomani huyo walimchukua mfungaji bora namba mbili katika Ligi Kuu ya Morocco, Axel Meye aliyefunga mabao 12 akiwa na klabu yake ya Ittihad Tanger.

Al Hilal walimsajili Meye kwa dau la Dola 800,000 (takriban Sh1.8 bilioni) huku pia wakimchukua mshambuliaji mwingine hatari wa AS Vita, Makabi Lilepo. “Hakuna timu ambayo haifungiki kila kitu kinawezekana kama tutakuwa na mpango mzuri wa kutafuta ushindi. Nafahamu mabadiliko yao Al Hilal sio timu ile ambayo tulikuwa tunaijua kutoka msimu uliopita. Msimu huu wamewekeza fedha kuleta wachezaji bora.

“Tunatakiwa kupambana na ubora waao. Hakuna kinachoshindikana hata sisi (Yanga) tuna kikosi bora, japo hatujatumia fedha kama wao,” alisema Nabi ambaye timu yake inampigia hesabu Mbrazili wa Singida BS, Dario Frederico atakayepishana na Jesus Moloko Yanga.