Nabi atimua staa kambini

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi hataki mchezo. Si unakumbuka aliwahi kuwachenjia, Michael Sarpong na Lamine Moro, sasa juzi kati kipa Ramadhani Kabwili aliingia kwenye 18 zake na kutimuliwa kambini na mabegi yake kabla ya mabosi wa klabu hiyo kuingilia kati fasta.

Kama ilivyokuwa kwa Lamine na Sarpong, waliozinguana na Nabi kwa utovu wa nidhamu, Kabwili naye alijikuta akitimuliwa kwa kilichoelezwa kutofautiana maneno na kocha Nabi, huku ikielezwa chanzo cha yote ni mkalimani aliyekuwa akiwasilisha maneno kwa wawili hao.

Si mnajua, Nabi anazungumza kwa ufasaha Kiarabu na Kifaransa, huku akikipiga kwa mbali Kiingereza, sasa juzi kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea kambini Avic Town, Kigamboni kipa huyo hakufurahishwa na kuwekwa nje wakati wenzake wakiendelea kukipiga uwanjani.

Inelezwa Kabwili alitoka nje wakati mwenzake, Faruk Shikhalo akibaki uwanjani na kocha kuanzisha mazoezi na kucheza na kumfanya kipa huyo namba tatu kumtumia mmoja ya wachezaji wanaoumika kama wakalimani baina ya kocha huyo na nyota wake kuulizia mbona amruhusu aingie kucheza.

Hata hivyo, inaelezwa aliyefikisha ujumbe kwa Nabi aliyakoroga kwa kufikisha sivyo na kumfanya kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Tunisia kuwaka na kumtuma mchezaji huyo kumweleza Kabwili afutike kambini fasta kabla mambo mengine hayajaharibika.

Mwanaspoti imepenyezewa taarifa zilizothibitishwa na baadhi ya viongozi tofauti kuwa, tayari jambo hilo limeshawekwa sawa baada ya kubaini kulikuwa na upotoshwaji wa ujumbe baina ya kocha na Kabwili na ndicho kilichomfanya kila mmoja kujisikia vibaya na kuchenjiana.

“Ilikuwepo sintofahamu baina ya watu watatu tofauti Nabi, Kabwili na mkalimani ambaye ni mchezaji mwenzake (jina limehifadhiwa), wakati huo Kabwili alikuwa nje alimwita mwenzake na kumuuliza kwa nini kocha hanipi nafasi ya kucheza mazoezini na kuomba amuulize,” alisema mmoja ya watu wa benchi la ufundi, aliyekataa kutajwa jina na aliongeza;

“Yule mchezaji ambaye ni mkalimani akaenda kumwambia kocha, Kabwili anasema kwa nini haumpangi, kocha akamjibu lakini mkalimani alirudisha majibu kwa Kabwili kuwa kocha kasema hana mpango na wewe na hakutumii kama vipi sepa, baada ya kauli hiyo basi Kabwili aliumia sana akasepa.”

Chanzo hicho kilisema; “Baadae ikagundulika kilichotokea ni kushindwana kuelewana lugha na sio kweli kama kocha alisema hamtaki Kabwili ndani ya timu, pia kipa huyo hakuwa anahoji kutochezeshwa kwenye mechi za ligi, ila mkalimani alipotosha.”

Chanzo kingine kilisema, mara baada ya sintofahamu hiyo viongozi waliamua kuingilia kati na kuwasikiliza wote watatu na kubaini kulikuwa na shida ya kimawasiliano kutokana na Nabi kwa kutofahamu kwake Kiingereza na wamepanga kesho (Jumatatu) kwenda Avic kulimaliza kabisa.

“Kabwili ameshaambiwa arejee kambini Jumatatu, ili kuendelea na mazoezi na wenzake, kwani jambo sio kubwa kama linavyokuzwa,” kilisema chanzo hicho kilichokiri Kabwili alitimka kambini, japo wachezaji wote walipewa mapumziko kabla ya kurudi kesho kujiandaa na mchezo wao na Ruvu Shooting utakaopigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mwanaspoti lilimtafuta Mkuu wa Idara ya Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ili kuthibitisha juu ya taarifa hiyo, naye alisema kwa kifupi “Suala la Kabwili tayari wameshalifanyia kazi kama uongozi na kipa huyo ni mchezaji wa Yanga.”

Bumbuli alipobanwa zaidi alisema kwa sasa wachezaji wapo mapumziko mafupi ya siku mbili na leo jioni au kesho asubuhi wanatakiwa kambini akiwamo Kabwili ili kuendelea na mikakati yao ya kukusanya pointi katika mechi zao tano zilizobaki Ligi Kuu na mchezo wao wa ASFC