Namna ya Simba, Yanga kutoboa ugenini CAF
Michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kwenye Uwanja wa Mkapa ilimalizika kwa matokeo tofauti wikiendi iliyopita na sasa kila mmoja anasubiri kuona ni kwa namna gani miamba hiyo ya soka nchini itatoboa ugenini.
Simba iliyocheza Ijumaa iliyopita ilipata kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Al Ahly ya Misri, huku Yanga ikiambulia suluhu kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Michezo yote miwili imekuwa na maswali mengi kutokana na timu zote kushindwa kuibuka na ushindi nyumbani.
Mashindano ya Afrika mara nyingi timu zimekuwa zikifaidika zaidi zinapocheza kwenye uwanja wa nyumbani, tofauti na zilivyo timu za Ulaya. Je, Simba na Yanga zitatoboa ugenini? Namna ya kufuzu ni hii hapa.
Yanga matatu, Simba moja
Kitendo cha Simba kupoteza kwa bao 1-0 kinazidi kuiweka timu hiyo kwenye wakati mgumu kwa kuwa itatakiwa kuibuka na ushindi kama huo ugenini ili iende kwenye matuta, lakini suluhu ya Yanga inaweza kuwa na faida kubwa kwao kwa kuwa inaweza kukaa nyuma na kuhakikisha timu yao hairuhusu bao lolote na kwenda kwenye mikwaju ya penalti.
Hivyo kwa Yanga wana mambo matatu ambayo ni faida kwao ambayo ni; kwanza sare ya mabao yoyote na pili ni ushindi, hivi vyote vitawapeleka nusu fainali wakati la tatu ni kulazimisha suluhu ugenini ambayo itawapeleka kwenye kupigiana matuta.
Hali ni tofauti kwa Simba. Wao wana jambo moja tu ambalo ni ushindi. Simba ni lazima ishinde ndio ipate chochote. Ikishinda 1-0 ndio itaingia katika kupigiana penalti. Ikishinda kwa tofauti ya mabao mawili ndio itatinga nusu fainali.
Inawezekana japo ngumu
Simba na Yanga zote zinaweza kuibuka na ushindi kwenye michezo ijayo kama zitafanya maandalizi mazuri kwenye kipindi cha wiki moja ambacho kimebaki kwa kuwa hakuna kinachoshindikana kwenye soka.
Kocha Benchikha wa Simba na Miguel Gamondi wa Yanga wamekiri mechi za nyumbani zilikuwa ngumu na hata za ugenini hazitakuwa rahisi, lakini wanaenda kujipanga na kurekebisha kila dosari ili wapindue meza ugenini kwani mechi hizo hazijaisha licha ya matokeo ya Kwa Mkapa.
Hata hivyo, Simba na Yanga zinapaswa kurekebisha kila dosari zilizoonekana kwenye mechi hizo za nyumbani, kwani ugenini kunaweza kuwa kugumu kwa rekodi na aina ya soka linalochezwa na timu wenyeji wanapokabiliana na wapinzani wakiwa nyumbani.
Mamelodi katika mechi tisa za CAF tangu Aprili mwaka jana imeshinda saba nyumbani na kutoka sare mbili bila kupoteza, ikifunga mabao 13 na kufungwa matatu tu, lakini Al Ahly tangu Mei mwaka jana katika mechi za mashindano yote ilizocheza haijapoteza zaidi ya kushinda 19 na sare tano.
Hata hivyo, mechi pekee iliyochezwa Saudi Arabia ikiwa ni ile ya Caf Super Cup wao wakiwa wenyeji ndio walipoteza kwa bao 1-0 mbele ya USM Alger ya Algeria iliyokuwa ikinolewa na Benchikha ambaye baada ya mchezo huo alijiuzulu na kuibukia Simba.
Mbinu za wageni
Staili ya kucheza kwa Mamelodi ilionyesha dhahiri kuwa waliiheshimu Yanga lakini wakiwa wanafahamu ni kitu gani wanataka, ndiyo maana muda mwingi walikuwa wakicheza kwenye eneo lao la ulinzi bila wasiwasi wowote ikiwataka Wananchi waende kufukuzia mpira, lakini Wanajangwani walionekana kutambua kuwa huo ulikuwa ni mtego.
Pamoja na kwamba Mamelodi iliongoza kwa umiliki wa mpira, lakini faida hiyo waliipata kwenye eneo lao na siyo lile la Yanga kwa kuwa ndiyo sehemu ambayo walikuwa inawapa uhuru wa kukaa na mpira kwa muda mrefu.
Vivyo hivyo, hata upande wa Simba, baada ya Ahly kufunga bao waliiachia Simba mpira na kurudi nyuma kujilinda.
Kilichoonekana kwenye mchezo huo ni tofauti ya ubora wa klabu hizo na hata kwa mchezaji mmoja mmoja huku uzoefu ndio ulioamua mechi, kwani Simba ilitengeneza nafasi nyingi, lakini ilishindwa kuzitumia na wenzao waliitumia moja na kuwatosha kutoka na ushindi wa kwanza ugenini dhidi ya Mnyama katika mechi zote za CAF walizowahi kukutana kuanzia mwaka 1985.
Tatizo la kutotumia nafasi zinazotengenezwa halipaswi kuridiwa ugenini Cairo na Pretoria Ijumaa hii.
Simba na Yanga zinapaswa kukumbua kwamba katika hatua hii ya michuano, nafasi zinazotengenezwa ni chache na zinapaswa kutumiwa. Makocha Benchikha na Gamondi ni lazima wafanyie kazi jambo hilo kwa sababu kufunga mabao ndio njia pekee ya kutoboa.
Simba kadi 17
Simba ndiyo timu inayoonekana kuwa na nidhamu mbovu zaidi baada ya kukusanya kadi za njano 17 hadi sasa kuanzia hatua ya makundi, huku kiungo wake Sadio Kanoute akiwa nazo nne.
Hii sio ishara nzuri ya nidhamu klabuni, lakini jambo la ajabu ni kwamba mechi ijayo zinakutana timu ya kwanza kwa kadi na ya pili kwa kuwa Ahly nayo inazo 14, ikiwa nafasi ya pili kwa nidhamu mbovu. Suala la kucheza kwa mbinu na nidhamu ni muhimu katika kusaka mafanikio kwa timu zote Simba na Yanga Ijumaa hii.
Yanga juu ya Mamelodi
Yanga imeonekana kucharuka ghafla na sasa inaongoza kwenye timu iliyopiga mashuti mengi kuanzia hatua ya makundi ikiwa ina wastani wa mashuti matano, nafasi ya pili inashika Mamelodi ikiwa na mashuti manne.
Hiki ni kitu cha kujivunia na kuongeza juhudi. Yanga inapaswa kuendeleza ubora huu na Simba pia inapaswa kuongeza umakini katika kujaribu kwa mashuti mara kwa mara kwa sababu bila ya kupiga shuti huwezi kufunga.
Katika mashindano hayo ya CAF msimu huu, Mamelodi inaongoza vipengele viwili muhimu baada ya mechi ya juzi, kipengele cha pasi nyingi ina wastani wa pasi 493 ikifuatiwa na Ahly 398, huku kwenye kipengele cha wastani wa umiliki ikikaa na mpira kwa asilimia 65.8 katika nafasi ya kwanza.
Mbinu ya Yanga kutokukimbiza kila mpira ilikuwa ni muhimu katika kutunza nguvu ya wachezaji wasichoke na inapaswa kutumika kiwerevu zaidi kule Pretoria ili kushinda ugenini.
Simba ilishambulia vyema nyumbani na inapaswa kucheza kama vile ugenini Cairo lakini kwa tahadhari.