Namungo yamtimua Maxime Kagera Sugar

Muktasari:

  • Maxime msimu huu wa 2020/21 ameiongoza Kagera Sugar mechi 23, ambapo amekusanya pointi 24 na kuiacha timu hiyo katika nafasi ya 13.

Mwanza. Kocha Mecky Maxime amethibitisha kuachana na timu ya Kagera Sugar  baadà ya kukaa meza moja na waliokuwa mabosi wake kwa madai ya mwenendo usioridhisha wa matokeo katika Ligi Kuu.

Maxime  msimu uliopita aliipa mafanikio Kagera Sugar kwa kumaliza nafasi ya tano na kuwindwa na Yanga, mabosi wa klabu hiyo walimpa mkataba wa miaka miwili ambao hata hivyo haujaweza kumalizika.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Maxime amethibitisha kuachana na timu hiyo, akifafanua kuwa tangu jana Ijumaa jioni aliketi meza moja na mabosi wake na kuajdiliana kuachana kwa amani.

Amesema sababu kubwa ya kufikia maamuzi hayo ni kutokana na matokeo kutoridhisha na kwamba kwa sasa yuko huru na kama kutatokea timu inayohitaji huduma yake anaikaribisha.

"Ni kweli kama ulivyosikia, tangu jana Ijumaa jioni niliongea na viongozi na leo tumeachana, kikubwa ni matokeo ila kama kina timu ije tufanye kazi" amesema Maxime.

Hatua hiyo imetokea ikiwa ni saa moja tu baada ya timu hiyo kukubali kipigo nyumbani cha bao 1-0 dhidi ya Namungo lakini ikiwa ni mechi ya pili mfululizo kufungwa hapo Kaitaba baada ya awali kufa kwa mabao 2-1 mbele ya Azam.