Ngushi aibeba Mashujaa, Coastal Union mambo magumu
Muktasari:
- Ushindi huo unaifanya Mashujaa kupaa mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 7 kwa kushinda mechi mbili na kutoa sare moja.
Dar es Salaam. Bao la mshambuliaji Crispin Ngushi,limetosha kuipa ushindi wa pili Mashujaa, ikiendeleza makali yake kwenye Ligi Kuu Bara ikiwalaza Coastal Union ya Tanga kwa bao 1-0.
Ngushi amefunga bao hilo pekee dakika ya 14 akipokea pasi ya beki wake Abderhman Mussa kisha mfungaji kuwatoka kiakili mabeki na kipa Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita Ley Matampi wa Coastal Union.
Ushindi huo unaifanya Mashujaa kupaa mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 7 kwa kushinda mechi mbili na kutoa sare moja.
Kipigo hicho cha Coastal Union kinaifanya timu hiyo kufikisha mechi mbili bila kupata ushindi ikibaki nafasi ya 13 na pointi yao moja iliyotokana na sare ya bao 1-1 iliyoipata dhidi ya KMC.
Kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, Coastal ikiwa mwenyeji imeonyesha kiwango cha kawaida ikikosa makali kwenye safu yao ya ushambuliaji na ulinzi pamoja na kumtumia kwa mara ya kwanza beki kisiki Lameck Lawi.
Ngushi ambaye ametua Mashujaa akitokea Coastal Union, ameendelea kuwa usajili mzuri kwa Wanajeshi hao akifunga bao la pili msimu huu ambapo kwenye mechi mbili alizofunga timu yake imeibuka na alama tatu.