Nkana yadidimiza ndoto za Namungo Afrika

Muktasari:

  • MCHEZO wa Kombe la Shirikisho Afrika uliozikutanisha timu za Nkana ya Zambia na Namungo ya Tanzania umemalizika kwa Nkana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 matokeo ambayo yamezima ndoto za Namungo kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

MCHEZO wa Kombe la Shirikisho Afrika uliozikutanisha timu za Nkana ya Zambia na Namungo ya Tanzania umemalizika kwa Nkana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 matokeo ambayo yamezima ndoto za Namungo kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Baada ya Namungo kupoteza mchezo huo wamebaki katika nafasi ya mwisho ya kundi lao D wakiwa wamecheza jumla ya mechi nne bila kupata alama wakifungwa 1-0 na Raja Casablanca ya Morocco, 2-0 na Pyramids ya Misri na 1-0 mara mbili na Nkana kwa maana ya nyumbani na ugenini na michezo ya kukamilisha ratiba Namungo itacheza na Pyramids ugenini na Raja Casablanca nyumbani mechi ambazo hata wakishinda hawatakwenda hatua inayofuata kwani wanazidiwa alama na vigogo hao walio juu yao.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote mbili kucheza kwa kujilinda na kushambulia kwa kustukiza huku wageni Namungo wakionekana kumiliki mpira kwa asilimia kubwa kuliko wenyeji Nkana hususani katikati ya kiwanja walipokuwa wakicheza Fredy Tangalo,Lucas Kikoti na Hamis Nyenye.

Baada ya kuona kuzidiwa, kocha mku wa Nkana Kelvin Kaindu aliamua kufanya mabadiliko dakika ya 26 kwa kumtoa Stephano Chulu na nafasi yake kuchukuliwa na Duke Abuya mabadiliko yaliyoipa nguvu Nkana na kuanza kulishambulia lango la Namungo mara kwa mara.

Mashambulizi yaliendelea kwa timu zote mbili zikitafuta bao la kuongoza lakini juhudi hizo ziligonga mwamba kwani mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika matokeo yalikuwa ni 0-0.

Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi ile ile na dakika ya 54 Nkana walifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Diamond Chikwekwe mfungaji wa bao pekee lililowapa ushindi kwenye mchezo wa awali uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa Aprili 4 na nafasi yake kuchukuliwa na Harisson Chisala.

Pia kwa upande wa Namungo kocha Hemed Morocco alimtoa Ibrahim Abdallah na nafasi yake kuchukuliwa na Sixtus Sabilo aliyeingia kuongeza kasi kwenye eneo la ushambuliaji akicheza kama winga wa kulia.

Dakika ya 71 Nkana walipata bao la kuongoza kupitia Freddy Tshimenga kwa aliyepiga shiti kali lililomshinda kudaka kipa wa Namungo, Jonathan Nahimana na kuzama nyavuni.

Bao hilo liliwapa nguvu Nkana na kuanza kushambulia lango la Namungo mara kwa mara huku wakifanya mabadiliko kwa kuwatoa Tshimenga, Mwinde na kuingia, Ackim Mumba na Jastine Mwanza sambamba na Namungo waliowatoa Lucas Kikoti, Jaffary Mohamed na nafasi zao kuchukuliwa na Adam Salamba na Stephene Duah.