Okra: Tulieni nakuja Simba

Monday June 27 2022
tulienipiic
By Mwandishi Wetu

SIMBA inafanya mambo yake kimyakimya na staa mwingine wa kigeni ambaye atakuja kufufua maisha mapya ya kikosi hicho ameshusha mkwara mzito ndani ya kikosi hicho.

Kiungo mchezeshaji kutoka Bechem United, Augustine Okrah amesema kuna asilimia 90 msimu ujao atakuja kuichezea Simba baada ya kukaribia kumalizana kila kitu na klabu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Ghana, Okrah alisema “Nitakuja Tanzania siku chache zijazo, naweza kusema kila kitu kimekwenda vizuri, unajua kama mchezaji unajisikia faraja ukifuatwa na klabu inayokuhitaji hadi ulipo, hii ni heshima kubwa.”

“Simba ni klabu kubwa ambayo kila chezaji mwenye ndoto za kufika mbali angetamani kuitumikia, nimekuwa nikiifuatilia, ina mashabiki wengi wanaoipenda klabu yao, sina wasiwasi kuja kuitumikia klabu kubwa kama hiyo.”

Aidha Okrah anayenukia kuchukua tuzo ya Kiungo Bora wa Ligi Kuu ya Ghana alisema ujio wake ndani ya Simba anataka kuendeleza msimu wake bora akitokea Bechem.

“Kabla ya yote mimi ni mchezaji ambaye najitambua, nafahamu nakwenda Simba ambayo ni wazi nitakutana na wachezaji wakubwa lakini nitatumia kipaji changu na juhudi zangu kupata nafasi, mimi sio mchezaji nitakayekubali kirahisi ushindani wa nafasi,” alisema.

Advertisement

Ingawa Simba inafanya siri usajili huo, lakini Okrah aliyefunga mabao 14 katika mechi 31 akiwa na ‘The Hunters’ anakuwa staa wa pili kumalizana na wekundu hao akitanguliwa na mshambuliaji Mzambia Moses Phiri aliyesaini mkataba wa miaka miwili.

Advertisement