Onyango ashtua Simba

Wednesday June 09 2021
onyangopic

MAMBO ni moto huko Msimbazi. Wakati Simba imeendelea kuwaongezea mikataba nyota wake akiwamo kipa, Beno Kakolanya aliyesaini mkataba wa miaka miwili, ishu ya beki kisiki, Joash Onyango, imepamba moto.

Onyango anayefahamika pia kwa utambulisho wa ‘Nusu Mtu Nusu Chuma’ kutokana na ungangari wake kazini, amestua baada ya kuzuka kwa tetesi za kutakiwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Kutokana na jambo hilo Mwanaspoti linafahamu kuwa, uongozi wa Simba umeitana na kufanya kikao cha kimya kimya ili kujadili suala la Onyango na maamuzi ambayo wamekubaliana si kumuuza bali ni kumuongeza mkataba mpya.

Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinaeleza tayari Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez amempa taarifa Onyango kupitia (Email), pamoja na wakala wake aliyopo Kenya juu ya nia yao hiyo.

“Tayari tumewataarifu Onyango na wakala wake kupitia barua pepe kuwa tunahitaji kumuongeza mkataba mpya wa miaka miwili ambao utaanza mara baada ya huu wa sasa kumalizika,”

“Mkataba wa awali ulikuwa wa miaka miwili ambao utamalizika mwisho wa msimu ujao lakini kutokana na kiwango bora alichoonyesha Onyango tumeamua kumuongeza mwingine wa miaka miwili ambao utamalizika 2024,” alisema amtoa taarifa na kuongeza.

Advertisement

“Tumefanya hivyo kutokana na timu kuhitaji mchango wake lakini kama kuna ambao watakuwa wanataka huduma yake tunaweza kuongea nao huku akiwa na mkataba mwingine wa Simba.”

Onyango alisajiliwa na Simba msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea, Gor Mahia ya Kenya lakini usajili wake ulizua mvutano wa pande mbili kati ya viongozi wa klabu hiyo, wengine wakitaka apewe wa muda mrefu na wengine wakitaka apewe mkataba wa muda mfupi wakiamini umri wake ni mkubwa.

onyangopicc

Jambo hilo lilipelekea mchezaji huyo kusaini mkataba tofauti na makubaliano ya kimaslahi ya awali lakini huenda sasa atakwenda kupata pesa ya maana kutokana na ubora wake alionyesha huku akiwa na ofa nyingine mkononi.

GOMES KUKOSEKANA

Katika hatua nyingine kikosi cha Simba kinarejea leo mazoezini baada ya mapumziko ya wiki moja mara baada ya kurejea kutokea Mwanza walipocheza mechi ya ligi dhidi ya Ruvu Shooting.

Wachezaji ambao hawapo katika majukumu ya timu zao za taifa wanatakiwa kurudi kambini leo (Jumanne), ili kuanza ratiba ya mazoezi ya ndani (Gym) na mengineyo ambayo yatasimamiwa na kocha wa viungo, Adel Zrane.

Advertisement