Onyango awawekea ngumu mastraika

BEKI wa Simba, Mkenya Joash Onyango amesema kazi yake ni moja tu akiwa uwanjani ni kuhakikisha washambuliaji wa upinzani hawapiti kirahisi mbele yake, ili kulinda usalama wa timu isifungwe mabao mengi kwa msimu huu.

Ameliambia Mwanaspoti online hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kwamba atajisikia mwenye furaha msimu ukiisha Simba ikiwa inaongoza kwa kuwa na idadi ndogo ya mabao ya kufungwa, lakini pia ikiwa kinara cha kufunga mabao mengi.

Amesema anafurahia kuifanya kazi yake kwa moyo kwa kuwa ndio kitu kilichomleta Tanzania, hivyo amejipanga kupambana hadi tone la mwisho kulinda heshima ya klabu yake kuwa bora kila idala.

"Simba ni timu yenye malengo makubwa kuanzia ligi kuu, Caf na Kombe la Shirikisho Afrika, kila mchezaji ana hamu ya kuona tunafikia malengo yetu, ndio maana upande wangu huwa nafurahia zaidi nikifanya kazi yenye kuwapa ugumu wapinzani wetu," amesema na ameongeza kuwa;

"Furaha yangu nikiwa uwanjani nikuwakaba wapinzani wetu kuona hawaambulii kitu, ingawa najua ligi ama mashindano tunayoyashirki yana upinzani wa hali ya ju, lakini ndio kazi lazima tupambane kwa kadri tuwezavyo," amesema.