Pacome, Aucho, Yao ndani Yanga ikiifuata Mamelodi

Kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua akiwa katika Uwanja wa Ndenge wa Kimataifa wa Julius Nyerere, leo alfajiri kwa ajili ya safari ya kwenda Afrika Kusini. 

Muktasari:

  • Nyota hao watatu waliukosa mchezo wa kwanza uliopigwa Jumamosi iliyopita, Machi 30, 2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi wakati Yanga ilipolazimishwa suluhu.

Yanga imeondoka nchini kuifuata Mamemolodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikiwa na msafara wa wachezaji 21 wakiwemo nyota wake watatu waliokuwa majeruhi viungo Pacome Zouzoua, Khalid Aucho na beki Atohoula Yao.

Nyota hao watatu waliukosa mchezo wa kwanza uliopigwa Jumamosi iliyopita, Machi 30, 2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi wakati Yanga ilipolazimishwa suluhu.

Msafara wa Yanga umeondoka nchini leo alfajiri kwa ndege ya Shirika la Malawi ukipitia jijini Blantyre kisha kuunganisha kwenda Afrika Kusini.

Katika msafara huo ambao pia wamo viongozi wa benchi la ufundi 12, Yanga imewajumuisha makipa wake watatu Djigui Diarra, Aboutwalib Mshery na Metacha Mnata.

Pia wamo mabeki wanane wakiongozwa na nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca',Gift Fredy, Kibwana Shomari, Lomalisa Mutambala, Nickson Kibabage na Yao.

Viungo 12 waliojumuishwa kwenye msafara huo ni Zawadi Mauya, Maxi Nzengeli, Salum Abubakar 'Sure boy', Augustine Okrah, Mahalatse Makudubela 'Skudu', Denis Nkane, Jonas Mkude, Farid Mussa, Stephanie Aziz KI, Pacome, Aucho na Mudathir Yahya wakati washambuliaji watatu ni Kennedy Musonda, Joseph Guede, Clement Mzize.

Yanga itashuka katika Uwanja wa Loftus Versfeld uliopo  Pretoria, Afrika Kusini Ijumaa, Aprili 5 kumalizana na Mamelodi kwenye mchezo ambao wana Jangwani watahitaji ushindi au sare yoyote ya mabao kufuzu nusu fainali ya mashindano hayo.