Kisa Marekani refa Msomali aondolewa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Mwamuzi huyo raia wa Somalia alitarajiwa kuandika historia ya kuwa Msomali wa kwanza kuchezesha michuano hiyo mikubwa duniani.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limesema kuwa Mwamuzi wa Somalia, Omar Abdulkadir Artan ameondolewa kuchezesha Fainali za kombe la Dunia 2026.
Taarifa ya FIFA amethibitisha kwamba Artan, amekataliwa kuingia Marekani baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami.
Baada ya mazungumzo na mamlaka za Marekani, FIFA imethibitisha kuwa Artan hatashiriki Kombe la Dunia la mwaka 2026.
"FIFA inaweza kuthib itisha kuwa mwamuzi Omar Abdulkadir Artan hataweza kushiriki mafunzo wala kuchezesha mechi za Kombe la Dunia 2026 baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani," imesema taarifa ya FIFA.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa FIFA haihusiki na taratibu za uhamiaji za nchi mwenyeji, ikiwamo utoaji wa viza, na kwamba mamlaka husika zimeeleza kuwa hali ya Artan haitabadilika kwa sasa.
Mamlaka za uhamiaji za Marekani hazijatoa sababu rasmi ya hatua hiyo, lakini Somalia ni miongoni mwa nchi zilizowekwa kwenye orodha ya marufuku ya usafiri iliyoanzishwa na utawala wa Rais Donald Trump.
Mshauri wa Serikali mjini Mogadishu amesema kwamba Artan ambaye angekuwa Msomali wa kwanza kuwa Mwamuzi katika fainali za kombe la Dunia alikuwa na visa halali ya kuingia Marekani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi Kazi cha Ikulu ya Marekani kinachosimamia Kombe la Dunia, Andrew Giuliani, ametetea uamuzi huo.
"Siwezi kuzungumzia taarifa za ndani kuhusu suala hilo, lakini naweza kusema ulikuwa uamuzi sahihi wa mamlaka za forodha na ulinzi wa mipaka, na ninaunga mkono uamuzi huo," amesema Giuliani.
Artan alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 walioteuliwa na FIFA kuchezesha mechi za Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika nchini Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.
Mwamuzi huyo amewahi kuchezesha mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na anatajwa kuwa mmoja wa waamuzi bora wanaochipukia barani Afrika.