Rekodi za Mnigeria Simba balaa!

WAKATI Yanga wakistua dirisha dogo kwa kumnasa mshambuliaji wa kimataifa wa raia wa Burundi, Fiston Abdoul Razak, watani wao wa jadi Simba nao ni kama walijibu mapigo kwa kushusha mtambo wa mabao, Junior Lokosa aliyewahi kutikisa Nigeria na kuwatoa udenda vigogo huko Norway, Bulgaria na China.

Lokosa linaweza kuwa jina geni kwa wadau wengi wa soka la Tanzania tofauti na hata Fiston ambaye anafahamika kutokana kocha wa timu ya taifa ya Burundi kumzungumzia wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars na pia taifa lake kuwa jirani na Tanzania.

Kabla ya mchezo ule wa kirafiki ambao Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0, lililofungwa na nyota wa Yanga, Saido Ntibazonkiza kocha wa Burundi, Jimmy Ndayizeye alikaririwa akidai anasikitika kumkosa mshambuliaji wake hatari, Fiston aliyekuwa amezuiwa na klabu yake ya ENPPI ya Misri na hapo ndipo alipoanza kuingia vichwani mwa Watanzania.

Zuio kama hilo pia liliiathiri Tanzania kwa kumkosa Himid Mao aliyekuwa akikipiga naye ndani ya klabu hiyo aliyowahi kuichezea kwa mkopo pia winga Shiza Kichuya.

Sasa achana na Fiston. Rekodi za Mnigeria, Lokosa anayetajwa kama mmoja wa washambuliaji hatari kwa sasa nchini Nigeria zinatisha na kama ataanza kuliamsha ndani ya kikosi cha Msimbazi, mashabiki wa klabu hiyo wajiandae tu kupata burudani maradufu kwani zile pasi za Clatous Chama na Luis Miquissone na krosi za kina Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe zitakuwa zikitumbukizwa vyema nyavuni.

Rekodi zinaonyesha kuwa Lokosa akiwa Kano Pillars ya kwao Nigeria ndani ya msimu wake wa kwanza tu, alicheza mechi 14 na kutupia nyavuni mabao matano hiyo ikiwa mwaka 2017.

Msimu uliofuata, 2018 aliendelea kuuwasha moto na kufunga mabao 14 katika michezo 15 tu na hapo ndipo vigogo wa klabu ya Ludogorets iliyokuwa ikishiriki Europa League, walipoamua kumtumia tiketi ya ndege na kumgharamikia kila kitu ili aende kufanya majaribio ya kujiunga na timu yao.

Hakuishia kufanya majaribio Bulgaria, lakini pia alienda Brann ya Norway kabla ya kurejea zake Nigeria, aliendelea pale pale Kano Pillars na kuanzia pale alipoishia na kumaliza msimu akiwa Mfungaji Bora katika Ligi Kuu ya Nigeria (NPFL) kwa kufunga mabao 19.

Baada ya msimu kumalizika aliamua kwenda zake China kujaribu tena bahati yake baada ya kukosa nafasi ya kujiunga na klabu zile mbili za Ulaya, ambazo aliitwa kwenda kufanya majaribio huko napo mambo hayakumwendea vizuri ndipo 2019 akasajiliwa na Esperance ya Tunisia.

Lokosa alishindwa kuonyesha makali yake akiwa na miamba hiyo ya soka la Tunisia ndani ya michezo 11 ya mashindano yote alitupia mabao mawili na ndipo Julai 30 mwaka jana klabu hiyo ilipotoa tamko la kuachana na mshambuliaji huyo na kuwa mchezaji huru.

Akiwa kwenye ubora wake Lokosa aliwahi kuitwa timu ya taifa la Nigeria kwenye kikosi cha awali kwa ajili ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia nchini Russia 2018 na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya DR Congo lakini hakubahatika kuwa miongoni mwa wachezaji 23 ambao walienda kuliwakilisha taifa hilo.

Huyo ndiye Lokosa ambaye awali Simba walimtaka kwa mkopo lakini akawagomea kabla ya kuafikiana na kuamua kumsajili kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi chao kitashiriki Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi ikipangwa Kundi A na timu za Al Ahly, As Vita na Al Merreikh.

Straika huyo ametua Msimbazi katika dirisha dogo sambamba na winga kutoka FC Platinum ya Zimbabwe, Perfect Chikwende na kiungo mkabaji kutoka Uganda, Taddeo Lwanga.