Rivers United wamsaka askari aliyewapiga Dar

Viongozi kadhaa wa timu ya Rivers United wametua katika kikosi cha Yanga wakimsaka askari aliyempiga mmoja wa viongozi wao.

Tukio hilo lilijiri jana wakati Yanga ikimaliza mazoezi yake ambapo baadhi ya viongozi wa Rivers walifika na kutaka kuonana na wenzao wa Yanga.

Viongozi hao wakiwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa wameonyesha kulalamikia hatua ya mmoja wa viongozi wao kupigwa wakati wa mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga uliopigwa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo wakiwa katika mazungumzo hayo mmoja wao alimtamkia Senzo kuwa hawajamuona askari ambaye alifanya tukio hilo wala vijana aliokuwa naye.

"Tulijua kwamba wale waliotupiga hawatakuwa wanaosafiri na timu, yule askari hayupo na wala wale vijana hatuwaoni," amesema mmoja wao akimueleza Senzo.

"Watu ambao hawasafiri ndio huwa wanafanya vurugu huwa hawajui kwamba wanawapa shida wenzao ambao wanasafiri ila walitufanyia unyama.

Hata hivyo Senzo akishirikiana na mjumbe wa kamati ya mashindano ya Yanga Mhandisi Hersi Said walilazimika kuwaomba radhi wakisema hawakujua kama matukio kama hayo yalifanyika.

"Tuwape pole kwa yote yaliyotokea askari huwa na kazi zao na kama kuna vitu vibaya mlifanyiwa havikutoka katika maelekezo ya Yanga ndio maana tulituma watu kuja kuwapokea na kuwapa ushirikiano," alijibu Senzo.