Robertinho atoa ramani ya vita Simba

KOCHA wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alirejea nchini siku kadhaa zilizopita na kuingia mazoezini, huku akiweka bayana ramani ya vita katika kuhakikisha timu inamaliza kibabe michuano ya Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC na Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi C.
Kocha huyo aliyeeenda Brazili kwa ishu zake binafsi, jana alionana na wachezaji akafanya kikao kifupi na wasaidizi wawili, Juma Mgunda na Ouanane Sellami ili kuelezwa kile kilichofanyika kwenye programu ya mazoezi aliyoacha kabla ya kuondoka.
Alikutana pia na wachezaji na kwenda mazoezini kwa maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Singida United utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Robertinho alisema amerejea Tanzania akiwa kwenye ubora zaidi ya awali na ana ramani nzuri ya kumaliza kibabe Ligi Kuu bara iliyosaliwa na mechi tisa pamoja na kuingia Ligi ya Mabingwa Afrika kibabe afanye vizuri zaidi ya alivyokuwa na Vipers ya Uganda.
Alisema amejipanga na wachezaji licha ya kuzidiwa alama sita na vinara Yanga   kubwa kwake ni kuona timu inabeba taji hilo na amekaa chini na wachezaji kama kundi na asilimia kubwa mmoja mmoja kuhakikisha wanaelewa anachotaka na mkakati wa pamoja utekelezwe kwa nguvu na morali kubwa ndani na nje ya uwanja.
“Tunahitaji kushinda ubingwa wa ligi ili kukamilisha hilo, lazima tushinde mechi zote tulizobaki nazo huku tukiangalia wapinzani wetu aina ya matokeo yao na uzuri wake tuna mchezo nao mmoja wa duru la pili, tukishinda tunazidi kupunguza pointi ilizonazo,” alisema Robertinho ambaye hivikaribuni alizinguana na mashabiki baada ya kumtoa Clatous Chama uwanjani.
“Tupo kwenye hatua nzuri katika FA, huku napo tukishinda michezo michache tunaweza kuchukua taji la ubingwa wa michuano hiyo na kufanikisha hilo tunahitaji kutengeneza morali na akili ya kila mchezaji.” Simba itavaana na Africans Sports katika mechi ya 16 Bora mwezi ujao.
Msimu uliopita timu hiyo ilikwamia nusu fainali na kuvuliwa taji na watani wao, Yanga kwa kufungwa bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Mei 28 mwaka jana jijini Mwanza.
“Nimepata nafasi ya kuangalia programu ya mazoezi niliyoacha wakati sipo kwenye timu ikiwemo utimamu wa miili wa wachezaji wapya, Ismail Sawadogo, Jean Baleke na Mohammed Mussa ambao sikupata muda wa kufanya nao mazoezi kwa pamoja kwa muda mrefu,” alisema Robertinho na kuongeza;
“Baada ya hapo napambana kutengeneza timu na kila mchezaji kuhakikisha inawezekana kucheza vizuri na kuvutia kila mechi na mwisho wa mchezo tunapata ushindi kwani ndio lengo kuu.”


KIMATAIFA
Katika hatua nyingine Robertinho ambaye wikichache zilizopita alionekana akiongeza utaalam nchini kwao, alisema kulingana na aina ya mazoezi na programu mbalimbali zilizo mbele yake wakati huu Simba itakuwa inapata matokeo mazuri kwenye michezo mikubwa.
Simba ipo makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa kundi moja na Raja Casabalanca ya Morocco, Vipers ya Uganda, timu aliyoinoa na kuifikia hapo kabla ya kuja Msimbazi pamoja na AC Horoya ya Guinea. Simba itaanza mechi za makundi wiki ijayon ugenini dhidi ya AC Horoya kabla ya kuikaribisha Raja Casablanca nyumbani wiki moja baadaye.
Robertinho alisema kama alivyoitengeneza Vipers na ikapata ushindi kwenye michezo dhidi ya timu kubwa kama TP Mazembe ugenini basi anaimani hata Simba itaweza kulifanya hilo.
“Nitatoa nafasi ya kucheza kwa kila mtu hata wale wapya na vijana,” aliongeza.