Saido: Bado nipo sana hapa Yanga

Monday July 19 2021
saido pic
By Khatimu Naheka

MSHAMBULIAJI wa Yanga Saido Ntibazonkiza amewashusha presha mashabiki wa Yanga akisema wala hana mpango wa kuondoka ndani ya timu hiyo kwasasa.

Saido ameyasema hayo kufuatia taharuki ya baadhi ya mashabiki waliotafsiri vibaya moja ya maandiko yake katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Katika mtandao wake akimalizia mechi ya mwisho ya ligi Saido aliandika kauli ya kuashiria kumalizika kwa msimu huku akiukaribisha msimu mwingine huku baadhi ya mashabiki wakitafsiri kama anaawaaga.

Akifafanua hilo Saido amesema bado yupo sana Yanga na kwamba hataweza kupingana na kila mtu anavyoweza kutafsiri mambo katika mitandao ya kijamii.

Saido ameongeza kwamba alisaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu  na kwamba sasa bado ana mwaka mzima ndani ya Yanga baada ya kumalizika msimu huu.

"Nipo sana hapa Yanga nina mwaka umebaki katika mkataba wangu,kilichotokea ni mashabiki baadhi kutafsiri tofauti katika kile nilichoandika,"amesema Saido.

Advertisement

"Ninachoshukuru tumemaliza msimu huu salama na sasa tutajipanga kwa mazuri zaidi kuelekea msimu ujao Mungu akipenda."

Advertisement