Sare zatawala Ligi Kuu, Mtibwa hali mbaya
Muktasari:
- JKT Tanzania ikiwa nyumbani imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC kwenye mchezo mkali na wa kuvutiwa uliopigwa Uwanja wa Meja Isamhuyo, Mbweni Jijini Dar es Salaam.
Mechi mbili za Ligi Kuu Bara zimemalizika kwa sare huku Mtibwa Sugar hali yao ikiendelea kuwa mbaya.
JKT Tanzania ikiwa nyumbani imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC kwenye mchezo mkali na wa kuvutiwa uliopigwa Uwanja wa Meja Isamhuyo, Mbweni Jijini Dar es Salaam.
Shaaban Iddi Chilunda, ambaye alitokea Simba kwenye dirisha dogo la Januari amefungua akaunti yake ya mabao kwenye ligi hiyo alipoisawazishia KMC katika dakika ya 40 ya mchezo, baada ya JKT kutangulia kwa bao la dakika ya 8 likifungwa na Najma Mangulu.
Sare hiyo imeipandisha JKT nafasi moja hadi ya 12, ikiishusha Tabora United, huku KMC ikibaki nafasi ya tano na pointi 24 kibindoni.
Mtibwa Sugar, imeendelea kubaki mkiani mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa baada ya michezo 17, huku jahazi lao likionekana kuendelea kuzama baada ya kutoka suluhu na Dodoma Jiji iliyofikisha pointi 20.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo kadhaa kupigwa, mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa ni kati ya Azam ambayo haijashinda michezo miwili mfululizo itakapokuwa mgeni wa Singida, iliyoshindwa kufanya vizuri kwenye michezo ya mzunguko wa pili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Ihefu tangu ilipohamia Singida ikitoka Mbarali Mbeya, watacheza mchezo wao wa kwanza kwenye Uwanja wa Liti dhidi ya Mashujaa, huku Geita Gold ikiwa Uwanja wa Nyakumbu kuvaana na Kagera Sugar.