Sarr awaachia kesi wazawa Simba
Muktasari:
- Bao pekee la Babacar Sarr limeipa Simba pointi tatu muhimu katika mchezo dhidi ya Geita Gold na kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na kuishusha Azam.
Dar es Salaam. Simba leo Februari 12, imeibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Geita Gold katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza huku kiungo Msenegali Babacar Sarr akiwaachia kesi mastaa wapya wazawa katika kikosi hicho.
Sarr ndiye aliipatia Simba bao la ushindi dakika ya 81, akifunga kwa mguu wa kulia akimalizia pasi ya kichwa iliyopigwa na Kibu Denis wote wawili wakiwa ndani ya boksi la 18 la Geita.
Bao hilo kwa Sarr limemfanya kufuata nyayo za wachezaji wengine wa kigeni waliosajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu, kwani Mgambia Pa Omari Jobe na Muivory Coast, Fredy Michael tayari walishafunga mabao kwenye ligi wakifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Tabora United, Simba iliposhinda 4-0, bao la kwanza likifungwa na Jobe, Sadio Kanote akitupia bao la pili, la tatu likifungwa na Che Malone Fondoh na Freddy kuweka nyavuni bao la nne.
Hiyo imekuwa kama salamu kwa wachezaji watatu wazawa waliosajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo, Salehe Karabaka aliyetokea JKU ya Zanzibar, Edwin Balua kutoka Tanzania Prisons na Ladack Chasambi kutoka Mtibwa Sugar ambao hawajafunga hadi sasa kwenye Ligi Kuu.
Hata hivyo, Karabaka ameonyesha utofauti dhidi ya Chasambi na Balua kwani licha ya kutofunga kwenye ligi lakini hadi sasa ameifungia Simba mabao mawili akianza kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya waajiri wake wa zamani (JKU), akiifungia Simba bao la tatu katika ushindi wa mabao 3-1 Januari Mosi mwaka huu.
Pia winga huyo mwenye spidi aliifungia Simba bao lingine Januari 31, kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), dhidi ya Tembo FC kutoka Tabora akiweka nyavuni bao la tatu katika ushindi wa 4-0. Mabao mengine ya Simba kwenye mechi hiyo yalifungwa na Luis Miquissone, Saidi Ntibazonkiza na Pa Omar Jobe 83.
Mchezo ujao Simba itacheza Alhamisi, Februari 15, mwaka huu dhidi ya JKT na itakuwa nafasi nyingine kwa Karabaka, Balua na Chasambi kujiuliza.
Simba kwa sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na alama 33 baada ya mechi 14, huku vinara ikiwa Yanga yenye alama 40 baada ya mechi 15.