Serikali kugharimia mashabiki wa Yanga kwenda Afrika Kusini

Muktasari:

  • Mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Mamelodi Sundowns na Yanga utachezwa katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria, Afrika Kusini, Aprili 5

Dar es Salaam. Mashabiki 48 wa Yanga wanaosafiri kwenda Afrika Kusini kushuhudia mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya timu yao na Mamelodi Sundowns itakayochezwa Ijumaa, Aprili 5 jijini Pretoria watagharimiwa na serikali, fedha za safari na za kujikimu.

Hayo yamesemwa leo na naibu waziri wa utamaduni, sanaa na michezo, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' wakati mashabiki hao wakianza safari hiyo.

"Asubuhi hii nimeshiriki kuwaaga wapenzi 48 wa klabu ya Yanga ambao wanaanza safari yao leo kwa basi kuelekea Pretoria, Afrika ya Kusini kushuhudia mchezo wa marudiano wa timu yetu hii dhidi ya Mamelodi Sundowns utakaochezwa Ijumaa ya tarehe 05/04.

"Safari hii itakayowawezesha wapenzi hawa kindakindaki wa Yanga kuishangilia timu yao mubashara wakiwa uwanjani imegharimiwa kwa asilimia mia na Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kwa vitendo na kutoa ushirikiano kwa uwekezaji binafsi kwenye sekta ya michezo," alisema Mwana FA.

Hii ni mara ya pili kwa serikali kugharimia mashabiki wa Yanga kwenda Afrika Kusini ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka jana ilipogharimia safari ya mashabiki wa timu hiyo kwenda kushuhudia mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya timu hiyo na  Marumo Gallants ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Rais wa Yanga, Hersi Said alisema kuwa klabu hiyo inaishukuru serikali kwa kugharimia mashabiki hao.

"Wizara itahudumia gharama zote za safari ya kuelekea Afrika Kusini yenye wanachama na mashabiki wetu 48 kuanzia nauli mpaka pesa ya kujikimu, hivyo sisi Young Africans tunaishukuru sana wizara. 

"Hapo mwanzo tulitangaza watu watakaosafiri walipaswa kuwa na shilingi laki 6 na tulipata watu 30. Niwahakikishie baada ya wizara kukubali kusafirisha wanachama na mashabiki wetu,zile laki 6 zitarudishwa kwa wenyewe.

"Niwatakie safari njema na nina imani safari yetu ya kurudi itakuwa nzuri kwa kuwa tutarudi tukiwa tayari tumeshafuzu hatua ya nusu fainal," alisema Hersi.

Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi iliyopita, Yanga ililazimishwa sare tasa hivyo inahitaji sare ya mabao au ushindi wa aina yoyote ili iweze kutinga hatua ya nusu fainali.