Simba Day hapatoshi Dar

Muktasari:

  • NI dakika 90 za nyota wa Simba hasa wale wapya kuthibitisha ubora wao kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo pamoja na wadau wa soka nchini wakati watakapoikaribisha TP Mazembe katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni mechi ya kadhimisha kilele cha tamasha la Simba Day leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

NI dakika 90 za nyota wa Simba hasa wale wapya kuthibitisha ubora wao kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo pamoja na wadau wa soka nchini wakati watakapoikaribisha TP Mazembe katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni mechi ya kadhimisha kilele cha tamasha la Simba Day leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Baada ya kukamilika kwa mchakato wa usajili pamoja na kambi ya kujiandaa na msimu ujao, ni wakati wa nyota wa Simba kuonyesha hadharani utayari wao kwa msimu mpya baada ya maboresho ya kikosi chao kukamilika.

Wakati sura za vipenzi viwili vya klabu hiyo, Clatous Chama na Luis Miquissone zikikosekana katika mchezo huo baada ya klabu hiyo kuwauza katika timu za RS Berkane na Al Ahly, ni fursa nzuri kwa nyota wapya waliojiunga na timu hiyo kudhihirisha kwa vitendo ndani ya uwanja kwamba Simba haikukosea kuwasajili na wanastahili kuvaa viatu vya wale walioondoka.

Nyota wapya ambao watatambulishwa rasmi ni Pape Sakho, Sadio Kanoute, Peter Banda, Duncan Nyoni, Enock Ibanga, Israel Patrick, Yusuph Mhilu, Kibu Denis, Jeremiah Kisubi, Abdulswamad Kassim na Jimmyson Mwanuke.

Lakini ukiachana na utamu wa ndani ya uwanja, kutakuwa na burudani za nje ya uwanja zitakazotolewa na kundi kubwa la wasanii wa muziki ambao wamepata fursa ya kutumbuiza wakiwemo wale wa bendi kongwe ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta.

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi alisema; “Kila mwaka tunajaribu kuongeza kiwango cha ufanisi na tamasha lenyewe kiujumla. Kama unavyojua mwaka tulifanya lakini mwaka huu tumesogeza juu kidogo kwanza kwa kuleta timu kubwa Afrika ambayo ni miongoni mwa timu kubwa Afrika tukiamini ni timu ambayo italeta ushindani katika Simba Day.


Tukio lenyewe tunataka liwe uzoefu mpya katika mpira. Tunataka mtu afike mapema lakini atapata burudani ambazo zitamfanya afurahie kwa muda wote atakaokuwa pale Uwanja wa Benjamin Mkapa,” alisema Nghambi.

Ni mechi ambayo benchi la ufundi la Simba chini ya Didier Gomes Da Rosa linaweza kutegua kitendawili cha mpangilio wa kikosi cha timu hiyo kitakavyokuwa kwa msimu ujao hasa kutokana na baadhi ya nafasi kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaowania namba ambao wengi wanaonekana kuwa na ubora

Nafasi ya winga ndio inayosubiriwa kwa hamu na wengi kuona nani ataanzishwa kati ya Bernard Morison, Banda, Duncan Nyoni, Sakho, Hassan Dilunga, Yusuph Mhilu na Jimson Mwanuke.


VITA YA KIUFUNDI

Mazembe wanatua leo mchana na kikosi kilichosheheni nyota wanaosifika kwa ubora wa kuzitafsiri vyema mbinu za makocha lakini pia ufanisi wa kujua kwa haraka wafanye nini katika wakati gani jambo ambalo limepelekea wawe wanafanya vizuri

“Mazembe wanashusha kikosi chao kamili na tayari wameshatoa orodha ambayo inajumuisha nyota wengi ambao wamekuwa chachu ya timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali,” alisema Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga.


REKODI YA KIBABE SIMBA DAY

Simba wamekuwa sio wanyonge katika mechi za kuadhimisha kilele cha tamasha lao na uthibitisho wa hilo ni kupata ushindi mara nyingi zaidi katika mechi hizo kuliko walizopoteza au kutoka sare.

Katika michezo 12 ya Simba Day ambayo Simba imecheza hapo nyuma, imeibuka na ushindi mara saba, kutoka sare mechi mbili na kupoteza michezo mitatu.

Imefunga jumla ya mabao 22 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tisa


KAGERE, AJIBU KIBOKO

Washambuliaji Medie Kagere na Ibrahim Ajibu hadi sasa ndio wanashikilia rekodi ya kupachika idadi kubwa ya mabao katika mechi za Simba Day kuliko wengine na inawezekana rekodi hiyo ikaboreshwa zaidi na wachezaji hao ama akapatikana mtu au watu wa kuifikia au kuivunja.

Kagere na Ajibu kila mmoja amefunga mabao matatu katika mechi hizo na anayewafuatia ni mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Bertram Mwombeki ambaye amefunga mabao mawili wakati wachezaji waliofunga bao mojamoja ni Chris Mugalu, Mohamed Ibrahim, Felix Sunzu, Awadh Juma, Hillary Echesa, Jonas Mkude, William Lucian, Emmanuel Okwi, Laudit Mavugo, Shiza Kichuya, Clatous Chama, Bernard Morrison, John Bocco na Charles Ilanfya


MWISHO WA UNYONGE

Ni mchezo ambao unaweza kumaliza au kuendeleza unyonge wa Simba mbele ya TP Mazembe kwani katika mara zote tano ambazo timu hizo zimewahi kukutana, Simba haijawahi kupata ushindi wowote dhidi ya mabingwa hao wa DR Congo. Katika mechi tano ambazo wamekutana, TP Mazembe imeibuka na ushindi mara tatu na zimetoka sare mara mbili, Simba ikifunga jumla ya mabao manne huku TP Mazembe ikipachika jumla ya mabao 10

Fuatilia mitandao ya kijamii ya Mwananchi tutakupa kila kitu kuhusiana na Simba Day usiku na mchana.