Simba kushusha mashine tatu mpya

Thursday January 07 2021
simba pic
By Thobias Sebastian

ACHANA na matokeo yao ya jana kwenye mchezo wao wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, unaambiwa mabosi wa Simba wamepanga kushusha mashine mpya tatu ili kukiboresha kikosi kabla dirisha dogo halijafungwa wiki ijayo. 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez aliliambia Mwanaspoti jana kuwa, kabla ya dirisha la usajili kufungwa kuna jambo ambalo watalifanya kwa baadhi ya wachezaji wapya ambao watakuwa wanawahitaji katika kikosi chao. 
“Kwa sasa ukiangalia kikosi chetu ni kipana na kina wachezaji wazuri, sioni sababu ya kumsajili mwingine ila tunakwenda kucheza Kombe la Mapinduzi na kuna baadhi ya wachezaji watakuja kufanya majaribio na kama watatufurahisha kidogo labda tunaweza kubadilisha mawazo,” alisema. 
“Wachezaji hao watatoka katika maeneo mbalimbali na kuna ambalo tutaangalia ni mahitaji ya timu ambayo kama itatokea kati ya hao waliokuja kufanya majaribio amekidhi tutabadilisha mawazo na kumsajili ili kuzidi kuimarisha timu yetu kuwa bora katika mashindano yote. 
“Miongoni mwa sababu inayoisaidia timu kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ni motisha ya pesa kama bonansi ambazo tunazitoa kwa wachezaji, ndio maana katika mchezo tuliwawekea wachezaji wetu bonansi kubwa ambayo hawakuwahi kukutana nayo.” 
Kikosi cha Simba kina wachezaji 10 wa kigeni kwa maana hiyo kama italazimika kusajili mgeni mwingine itamuacha mmoja kati ya walionao au kuwa naye bila ya kumtumia katika mechi. 
Wakati Barbara akieleza kuwa kuna baadhi ya wachezaji watatua kufanya majaribio, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ aliwahi kukaririwa akieleza wamejipanga kushusha wachezaji wa maana wa daraja la juu. 
TADDEO KUTUMIKA MAPINDUZI 
Barbara alisema kukosekana kwa mchezaji wao mpya kiungo mkabaji, Taddeo Lwanga ni kutokana na kuguua na juzi (Jumatatu), alifanya vipimo vya mwisho ambavyo vilitoka vizuri na ataanza kutumika katika Kombe la Mapinduzi. 

simba picc


“Taddeo alikuwa anakosekana uwanjani kwa kuwa alikuwa ni mgonjwa, lakini matibabu yake yamekwenda vizuri na wapenzi pamoja na mashabiki ambao wamekuwa wakimuulizia mara kwa mara wataanza kumuona katika Kombe la Mapinduzi ambalo tayari limeanza,” alisema. 
“Kuhusu vibali vya kazi na vingine vyote kama ITC tayari tumeshavipata na tumekamilisha kila kitu na kazi imebaki kuona namna gani tunaweza kumtumia katika mashindano yote ambayo yapo mbele yetu.” Taddeo hajatumika katika mechi yoyote tangu kusajiliwa na Simba watacheza mchezo wa kwanza wa Mapinduzi, Ijumaa dhidi ya Chipukizi.

Advertisement