Simba noma, washusha straika, awaachia Yanga manyoya

MWANANCHI limemnasa straika wa Mbeya City, Kibu Denis juzi saa 4:00 asubuhi akitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tanzania (JNIA) kuja kumaliza dili lake na Simba.

Mwananchi ambalo liliweka kambi katika uwanja huo lilimshuhudia Kibu akishuka kwenye ndege akiwa amevaa sweta jeusi lenye michirizi mieupe, kofia, barakoa, suruali nyeusi na viatu rangi ya udongo.

Simba kama wakimalizana na Kibu atakuwa mchezaji wa nne mzawa baada ya awali kuanza na kipa wa Tanzania Prisons, Jeremia Kisubi; beki wa kulia wa KMC, Israel Patrick Mwenda na winga wa Gwambina, Jimson Mwanuke.

Mara baada ya kutua alipokewa harakaharaka kisha kufichwa katika gari aina ya Toyota Crown rangi nyeusi iliyokuwa na vioo vyeusi ambavyo sio rahisi kumuona aliyekuwa ndani.

Kabla ya Kibu kuingia katika gari hiyo alipata nafasi kwa ufupi kuliambia Mwanaspoti kuwa: “Khaaa! Mbona hili jambo tumelifanya kwa usiri mkubwa na linaenda kimyakimya. Ok! Niache kwanza niende kukamilisha jambo langu kisha tutawasiliana.” Kibu alisema hayo akiingia kwenye gari na kushusha vioo kwenda zake.

Mwanaspoti linafahamu mchezaji huyo mara baada ya kumaliza mechi juzi Jumapili aliitwa na viongozi wa Mbeya City ambao walimueleza kuwa wapo tayari kumpa mkataba mpya.

Kibu baada ya kuambiwa hivyo na viongozi wa Mbeya City, aliwaeleza wampe muda ambao tayari alishasetiwa na watu wa Yanga ambao walimpelekea mkataba hotelini, lakini hakuusaini.

Habari zinasema kwamba baada ya kukutana na watu wa Yanga, Kibu aliwavutia waya mabosi wa Simba na kuwaeleza kuhusiana na hali hiyo ndipo wakamtumia tiketi ya ndege haraka akatua Dar es Salaam jana.

Awali, Mwanaspoti lilikujuza kuwa mchezaji huyo alishakuja Dar na kufichwa katika moja ya hoteli, na alikubaliana kila kitu na Simba kilichobaki ilikuwa ni kusaini mkataba tu ambao ndio jana alikuja kukamilisha.

Kibu aliliambia Mwanaspoti, baada ya ligi kumalizika ndio atafanya uamuzi wa mahala atakapokwenda kucheza msimu ujao au kubaki katika kikosi cha Mbeya City.

Katika hatua nyingine, Mwanaspoti limejiridhisha kuwa benchi la ufundi la Simba chini ya makocha Didier Gomes na msaidizi wake, Selemani Matola wamekuwa wakivutiwa na Kibu na hata lilipofika suala la usajili wake lilipitishwa moja kwa moja.

Gomes anaamini kwamba Kibu ndiye mbadala sahihi wa Meddie Kagere kwa sasa na ni aina ya wachezaji wazawa anaowapenda.

Mchezaji huyo mwenye rasta alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Biashara United na kuibakisha timu ya Mbeya City kwenye Ligi Kuu msimu ujao licha ya awali kuwa katika wakati mgumu wa kushuka.

Katika orodha ya wafungaji msimu huu, Kibu amefunga mabao saba nyuma tisa ya yale ya kinara, John Bocco, wa Simba aliyemaliza na mabao 16.

Dirisha la usajili wa wachezaji lilifunguliwa rasmi Julai 19 na litafungwa Agosti 31, kwa kila timu kupata nafasi ya kuongeza majembe mapya na kutema wanaowataka.

Gomes alisema watatumia dirisha hilo kusajili wakilenga mashindano ya ndani ikiwemo kuchukua tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alisema kwa wapinzani wao, Yanga, kuna wachezaji wengi wazuri na wazawa, lakini mipango yao ilivyo hawatasajili mchezaji yeyote kutoka katika timu hiyo pengine kama ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita.

“Katika ligi nimeona wachezaji wengi wazawa kutoka katika timu tofauti na kuna baadhi tutawapa nafasi ya kusajili, lakini tutafanya pia usajili wa wachezaji kutoka nje ya Tanzania,” alisema Gomes.

Kocha huyo aliongeza kuwa msimu ulikuwa bora kwake katika mashindano ya ndani na kwa maana hiyo hawatakuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi kwa maana ya kuingiza wachezaji wapya na kuwaacha wengi.