Simba SC, Yanga zapewa mchongo

Gomes kuisapraizi Al Ahly Cairo

SIMBA imerejea jana mchana kutoka Cairo, Misri ilipoenda kuchezea kipigo cha bao 1-0 mbele ya wenyeji wao Al Ahly katika mechi ya kufungia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini huku nyuma benchi la ufundi la timu hiyo likapewa mchongo ili kutisha zaidi kwenye ligi hiyo.

Sio kwa wawakilishi hao wa nchi tu inayosubiri kujua itacheza na nani hatua ya robo fainali itakayopangwa Aprili 30, lakini hata vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga nao wamepewa mchongo wa kijanja kama kweli inataka kupata heshima kubwa kwenye soka la Afrika.

Mchongo huo, umetolewa na nyota za zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba nchini na barani Ulaya, Sunday Manara ‘Computer’, aliyesema ili Simba ifike mbali zaidi kwenye mechi za CAF ni lazima iitazame safu yake ya ushambuliaji, kwani wasipojipanga vyema itawaangusha Afrika.

Kwa Yanga hii, mtaumia

Akizungumza na Mwanaspoti, Manara alisema, hatua waliyofikia Simba inatakiwa kuungwa mkono na kila mwanamichezo bila ya kujali ushabiki, lakini benchi la ufundi la timu hiyo lazima lirekebishe safu yao ya ushambuliaji.

Alisema licha ya kucheza vizuri juzi dhidi ya Al Ahly, lakini washambuliaji walikosa umakini na Kocha Didier Gomes alitazame hilo kabla ya mechi zao zijazo za robo fainali ambazo huwa ngumu na za mtoano.

“Simba imecheza vizuri sana na kwa nidhamu ya hali ya juu ikiwa ugenini na ilionyesha ukomavu mkali hata Al Ahly hawakuamini matokeo hayo.

“Ni heshima kubwa kwa nchi na hata sisi Yanga tujitahidi kuangalia namna wenzetu wamepata mafanikio basi na sisi tutumie mafanikio yao kujijenga zaidi,” alisema Manara.

Alisema kuelekea hatua zijazo Simba wanatakiwa waongeza uimara wao kimwili (fitness) na kumtolea mfano Luis Miquissone, aliyedai alishindwa kufurukuta katika mchezo huo kutokana na akiguswa kidogo tu anatoka nje.

“Fitinesi ni muhimu sana kwa wachezaji, hata Luis jana akiwekewa mwili tu kashadondoka nje hiyo ni shida Simba wajitahidi sana kuliangalia hilo, pia ni lazima Kocha Gomes aimarishe safu yake ya ushambuliaji inapoteza nafasi nyingi za mabao ambayo kwa hatua iliyopo ni muhimu mno.”


AIFUNDA YANGA

Aidha aliitaka Yanga kutumia nafasi watakayopata ya uwakilishi wa nchi kupitia mgongo wa Simba kuandaa kikosi bora kitakacholeta ushindani kama watani wao.

“Yanga waige sana mfano wa Simba, wafanye usajili mzuri na wachezaji wanaojulikana wataleta ushindani ndani ya timu ili tufanye vizuri mwakani kama Simba walivyofanya.”