Simba yaishika pabaya Kaizer Chiefs

MSAFARA wa Simba wa watu wasiopungua 40 ukiwa Johannesburg, Afrika Kusini tayari kwa maandalizi ya mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs utakaochezwa katika Uwanja wa FNB ‘Soccer City’ uliopo jijini humo, Jumamosi Mei 15.

Wakati Simba wakitua, rekodi ya Kaizer Chiefs pindi wanapokuwa nyumbani na nyakati ngumu ambayo wenyeji wao wanakabiliana nayo kwa sasa, inawaweka katika nafasi nzuri wawakilishi hao wa Tanzania, kupata matokeo mazuri ambayo yanaweza kuwarahisishia mpango wao wa kutinga nusu fainali za michuano hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa Uwanja wa Soccer City ambao utatumika kwa mechi hiyo ya ugenini ya Simba, umekuwa na nuksi kwa wenyeji Kaizer Chiefs kwani wamekuwa hawapati matokeo ya kuridhissha katika mechi za mashindano mbalimbali wanayochezea katika uwanja huo.

Msimu huu katika mechi 25 za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika walizocheza katika uwanja huo, wamepata ushindi mara sita tu huku wakitoka sare mara 11 na kupoteza michezo nane.

Katika hali ya kushangaza, Kaizer Chiefs pindi wanapokuwa nyumbani, wapinzani huwa na uwezekano mkubwa wa kufunga mabao kuliko wao kufumania nyavu za upande wa pili.

Kaizer Chiefs katika mechi zake 25 ilizocheza uwanja wa nyumbani msimu huu, imefunga jumla ya mabao 22 tu ikiwa ni wastani wa bao 0.88 kwa kila mchezo wakati yenyewe imefungwa mabao 25, ikiwa ni wastani wa bao moja kwa kila mchezo.

Kwenye Ligi ya Mabingwa pekee, Kaizer Chiefs wameibuka na ushindi mara mbili kati ya mechi tano walizocheza msimu huu huku wakitoka sare tatu, wakifunga mabao matatu tu ikiwa ni wastani wa bao 0.6 kwa kila mechi ingawa haijaruhusu bao.

Pamoja na takwimu hizo zisizovutia za Kaizer Chiefs, kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa alisema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu

“Timu zote katika mashindano haya ni imara na tunaipa heshima kubwa Kaizer Chiefs lakini tuna hamu na tunataka kufika hatua za juu katika haya mashindano na tuko tayari kucheza nao.

Itakuwa ni mechi ngumu lakini tuna muda wa kutosha kujiandaa, tunatakiwa kuelekeza akili yetu katika mechi hii na naamini tuko tayari kufika mbali kwenye haya mashindano,” alitamba Gomes

Ukiweka kando takwimu hizo zisizoridhisha kwa upande wa Kaizer Chiefs, timu hiyo ya Afrika Kusini inakutana na Simba ikiwa inakabiliwa na ratiba ngumu pamoja na changamoto ya majeruhi, jambo linaloweza kuwapa faida wawakilishi wa Tanzania dhidi yao.

Wakiwa tayari wanamkosa staa wao Khama Billiat ambaye ana majeraha ya kifundo, timu hiyo huenda ikawakosa wachezaji wake wanne tegemezi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Simba ikiwa hawatopona kwa wakwati.

Nyota hao ni makipa wawili chaguo la kwanza, Itumeleng Khune ambaye bado hajapona majeraha ya bega na Daniel Akpeyi ambaye ameumia kichwani, beki Eric Mathoho aliyeumia enka ambaye atakuwa nje kwa siku 10 na kiungo Lebogang Lesako atakakuwa nje kwa muda wa wiki mbili kutokana na majeraha ya goti.

Mbali na changamoto ya majeruhi, Kaizer Chiefs pia wanakabiliwa na ratiba ngumu ambayo haiwapi muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya kuvaa na Simba ambayo inaingia katika mechi hiyo ikiwa na mapumziko ya wiki nzima.

Mchezo dhidi ya Simba utakuwa ni wa sita kwa Kaizer Chiefs kucheza ndani ya muda wa siku 21 ikiwa na wastani wa kupumzika na kufanya maandalizi ya mchezo mwingine kwa muda wa siku tatukutoka mechi moja hadi nyingine.

Kocha wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt ameeleza kuwa changamoto ya ratiba na majereha inamuweka katika wakati mgumu kuelekea mchezo huo dhidi ya Simba.