Simba yalazimisha sare ya mabao 2-2

SIMBA jana ililazimisha sare ya mabao 2-2 ugenini mbele ya wenyeji Power Dynamos mjini Ndola, Zambia kazi kubwa ikifanywa na Clatous Chama aliyefunga mabao  mawili na kuiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi kama itapata ushindi wowote nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mnyama alipata sare hiyo kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Chama ambaye ni Mzambia akitumia uzoefu kufunga mabao katika kipindi cha pili akichomoa mabao ya Dynamos.

Joshua Mutale aliitanguliza Dynamos kwa bao la dakika 29 akipiga mpira uliosindikizwa wavuni na kipa aliyedaka kwa mara ya kwanza mechi za mashindano akiwa na Simba, Ayoub Lakred, bao lililodumu hadi mapumziko kabla ya Chama kuchomoa katika dakika ya 60.

Simba iliendelea kushambulia muda mrefu, lakini dakika ya 77 ikatunguliwa bao la pili kupitia kwa Cephs Mulombwa na wakati Wazambia wakiamini wameichapa Simba, Chama tena akafunga la kusawzisha dakika za lalasalama na kufanya matokeo kuwa 2-2.

Simba inahitaji ushindi wowote kutinga makundi kwa mara ya nne kwenye michuano hiyo tangu 2018, lakini ikiwa na kazi ya kuhakikisha haifanyi makosa kama ilivyotokea kwenye mchezo wa jana ambao uliwafanya Wazambia watawale muda mrefu.


AKILI YA ROBERTINHO

Kama kuna kitu ambacho Simba ilipatia ni uamuzi mzuri wa uteuzi wa kikosi cha kwanza uliofanywa na Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’. kocha huyo alipatia kila kitu. Moses Phiri ni Mzambia. Mpinzani alikuwa Mzambia.

Phiri ni moja kati ya washambuliaji wenye kila kitu. Kumuanzisha ulikuwa uamuzi sahihi, lakini dakika 45 za kwanza ni kama alikuwa mtalii uwanjani. Hakukuwa na presha kubwa kutoka kwake kwenda kwa mabeki wa Dynamos. Ni kama dakika 45 zote alikuwa anarukaruka tu uwanjani.

Washambuliaji wana faida moja tu kubwa. Anaweza kucheza ujinga kipindi cha kwanza, lakini akafunga kipindi cha pili na kuwafuta machozi mashabiki. Mchezaji kama Phiri alipaswa kufanya makubwa kipindi cha kwanza. Kelele zimekuwa nyingi sana juu yake.

Mashabiki wengi wa Simba wanadhani kocha huwa anambania kwa kumuweka benchi. Wengi wanaamini ana uwezo mkubwa. Ana uwezo wa kuibeba Simba. Mechi kama hizi mara zote ndizo ni za kutengeneza heshima. Mechi za kutengeneza imani kwa kocha na mashabiki.

Simba na Yanga huwa hazina uvumilivu wa muda mrefu. Ni aina ya timu zinazotaka matokeo chanya mapema. Kwa dakika 45 za kwanza, kiukweli Moses Phiri amewaangusha Msimbazi. Alikuwa anarukaruka tu. Najua na wewe ulitazama mechi, naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba ya simu hapo chini. Nileeze tu namna ulivyoona kiwango chake dhidi ya Wazambia na hasa kipindi cha kwanza.


AYOUB PRESHA TU

Kwa mara ya kwanza nimemtazama kipa mpya wa Simba, Ayoub dhidi ya Dynamos. Simba wamelamba dume. Pamoja na kufungwa nyavu zake, lakini unaona sifa zote za kipa bora ndani yake. Uwezo wa kuongea na mabeki wake ni wa hali ya juu. Ugawaji wa mipira ni levo nyingine. Hana papara langoni, miguu yake ni ufundi mtupu. Ayoub Lakred ni fundi kwelikweli. Hapa Simba wamepata mtu ambaye Aishi Manula anapokosekana kuna mtu wa kuziba pengo lake.

Bado Manula atabaki kuwa kipa bora kuzalishwa nchini miaka 10 ya hivi karibuni, lakini Simba wanaonekana watakuwa imara pale anapokosekana. Ayoub ameonyesha uwezo mkubwa na hasa dakika 45 za kwanza kwenye mechezo wa jana dhidi Dynamos pale nchini Zambia.

Aishi ni kipa aliyepitia mikikimikiki mingi ya nje na ndani ya uwanja. Ni ngumu sana kumpeleka benchi kirahisi, lakini Ayoub anajua. Huyu Mmorocco anajua sana mpira na Simba wamefanya uamuzi mzuri kumsajili. Kufungwa kwenye mpira sio uwezo tu wa kipa, ni uwajibikaji wa kila idara. Sina lawama yotote kwake. Ni suala la muda tu.

Atakuja kuimbwa muda sio mrefu. Najua na wewe unalipata nafasi ya kutazama mechi  hebu niambie namna ulivyomtazama kipa mpya wa Simba, Ayoub. Nitumie maoni yako kwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba ya simu hapo chini. Niambie umeona nini kwa kipa mpya wa Simba?


CHAMA HATARI

Mwamba wa Lusaka, Chama alikuwa Levy Mwanawasa Stadium. Sio yule ambaye nimezowea kumuona Benjamin Mkapa Stadium. Nadhani amebarikiwa akiwa kwa Mkapa kuliko uwanja mwingine wowote. Uzuri wake ni mmoja tu. Kuna bao katupia. Ni bao muhimu sana ambalo Simba walilihitaji. Haya ni aina ya mabao ambayo hubaki kama kumbukumbu kwa mashabiki wa soka maishani.

Ujio wa Jean Baleke umeleta tofauti kubwa Simba kiuchezaji. Chama anapewa sifa kwa kufunga tu, lakini shughuli kubwa ilikuwa kwa Baleke. Simba ni wakubwa sana Afrika kwa sasa hizi mechi dhidi ya timu kama Dynamos zinapaswa kuwa nyepesi. Lakini pomoja na yote, bado Simba wameonyesha ukomavu mkubwa dimbani jana. Wameonyesha utu uzima. Ujio wa Saido Ntibazonkiza na Baleke kipindi cha pili ulibadilisha kila kitu. Nadhani mechi ya marudiano, Ntibanzokinza na Baleke wanastahili kuanza. Umewatazama vizuri jana? Naomba maoni yako juu ya Baleke na Ntiba kupitia namba ya simu hapo chini.

Wale Simba wa kipindi cha pili jana ni kama Real Madrid. Ni kama unatazama Manchester City ya Pep Guardiola. Ule moto wakiwapelekea Dynamos kwa Mkapa mtu atakufa mapema tu. Hakuna lawana yoyote kwa Robertinho. Alifanya kila kitu sawa. Kosa la mwisho la kipa Ayoub liliwaangusha Simba. Ingawa kwangu, Ayoub anabaki kuwa kipa mwenye uwezo mkubwa na naona atawasaidia Simba msimu huu.

Kuna namna bao la pili liliwarudisha Simba nyuma, lakini bado walikuwa na mchezo mzuri. Simba wanajua namna ya kutinga hatua ya makundi Afrika. Nawaona wakimpelekea mtu pumzi ya moto kwa Mkapa. Bado naiona nafasi kubwa ya Simba wakiwa nyumabani. Bado nawaona Simba wakifuzu mapema tu Dar.

Simba iliyoanza jana: Lakred, Kapombe, Tshabalala, Malone, Inonga, Kanoute, Kibu, Mzamiru, Phiri, Chama na Onana.