Simba yamjaza hofu kiungo Kaizer Chiefs


Muktasari:

  • Kiungo Dumsani Zuma ametishwa na ubabe wa Simba inapokuwa nyumbani na ameitaka timu yake Kaizer Chiefs kuhakikisha inapata ushindi mkubwa nyumbani kesho watakapokutana ili wasiwe na wakati mgumu ugenini.

Kiungo Dumsani Zuma ametishwa na ubabe wa Simba inapokuwa nyumbani na ameitaka timu yake Kaizer Chiefs kuhakikisha inapata ushindi mkubwa nyumbani kesho watakapokutana ili wasiwe na wakati mgumu ugenini.

Kaizer Chiefs itaikaribisha Simba katika Uwanja wa FNB uliopo Johannesburg kabla ya timu hizo kurudiana jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ijayo ambapo mshindi wa jumla atatinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kukutana na mshindi wa jumla kati ya Wydad Casablanca na MC Ager.

Zuma anaamini kwamba njia pekee kwa Kaizer Chiefs kuitoa Simba ni kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao kesho vinginevyo watakuwa na wakati mgumu pindi watakapokabiliana na wawakilishi hao wa Tanzania katika mechi ya marudiano itakayochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi, Mei 22.

"Tunaweza kupata matokeo chanya. Tunajua haitokuwa mechi rahisi lakini tunatakiwa faida ya kucheza uwanja wa nyumbani kwa sababu ni kazi ngumu kucheza ugenini. Tunatakiwa kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao ili kufanya mambo yawe rahisi katika mechi ya marudiano.Hatupo katika hatua hii kukamilisha idadi bali tunatakiwa kwenda hatua za juu zaidi katika haya mashindano," alisema Zumba.

Simba imekuwa ikifanya vyema katika mechi za kimataifa pindi inapocheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo kwa muda mrefu haijapoteza mchezo uwanjani hapo.

Mara ya mwisho kwa Simba kupoteza mechi ya kimataifa nyumbani ilikuwa ni Februari 17, 2013 walipofungwa bao 1-0 na Recreativo Do Libolo ya Angola katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tangu hapo, Simba imecheza jumla ya mechi 14 za amshindano ya klabu Afrika, ikipata ushindi mara 10 na kutoka sare nne, ikifunga jumla ya mabao 32 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba tu.