Son awavuruga Mourinho, Solskjaer

Son awavuruga Mourinho, Solskjaer

Muktasari:

  • Jose Mourinho amemshukia kocha Ole Gunnar Solskjaer baada ya wawili hao kukutana katika mlango wa kuingilia vyumbani ulipomalizika mchezo wa timu zao, juzi usiku.

London, England. Jose Mourinho amemshukia kocha Ole Gunnar Solskjaer baada ya wawili hao kukutana katika mlango wa kuingilia vyumbani ulipomalizika mchezo wa timu zao, juzi usiku.

Kocha huyo wa Tottenham alikasirika baada ya Solskjaer kumshutumu Son Heung-min kwa kumrubuni mwamuzi wakati wa bao la Edinson Cavani, ambalo liliangaliwa na VAR na kugundulika kuwa raia huyo wa Korea Kusini aligongwa usoni na Scott McTominay.

Kocha wa Manchester Unirted, Solskjaer alisema: “Kama Son angeendelea kubaki chini kwa dakika tatu na kuhitaji wachezaji wenzake 10 waliobaki kumsaidia kunyanyuka, asingeweza kupata chakula chochote. Mchezo kwa sasa unapoteza mwelekeo.”

Lakini kocha wa zamani wa Man United, Mourinho alimjibu kocha mwenzake huyo na kuwaambia waandishi wa habari: “Ninachoweza kusema ni kwamba Sonny ana bahati sana kuwa baba yake ni mtu mzuri kuliko Ole.”

Cavani alidhani kuwa ameiandikia Man United bao la kuongoza, wakati alipomalizia vizuri kambani mpira wa mwisho dakika ya 33.

Lakini mwamuzi Chris Kavanagh alilikataa bao hilo baada ya kurejea katika picha za marudio ya VAR, baada ya kushauriwa kuangalia katika runinga ambayo imewekwa uwanjani.

Ulionekana kama uamuzi wa kuumiza na Mashetani Wekundu kujikuta wakiwa nyuma dakika saba baadaye kupitia kwa Son, ambaye alifunga kwa shuti na kuitanguliza Spurs.

Kocha wa miamba ya Old Trafford, Solskjaer, licha ya timu yake kubadilika na kupata ushindi kipindi cha pili, bado alikuwa na hasira na tukio la bao lililokataliwa.

Kocha huyo raia wa Norway alinukuliwa akisema katika runinga mara baada ya mchezo huo kumalizika: “Lilikuwa ni bao zuri kabisa. Hatukudanganya. Mwamuzi alidanganywa.”

Maoni hayo ndiyo yaliyomuibua Mourinho na kuwashutumu waamuzi waliokuwepo katika uwanja wakati wakimhoji kwa kutomuuliza kuhusu tukio hilo, licha ya kuwa hawakuwa wameona video hiyo.

Mourinho alisema: “Nimeshangazwa, nimeshangazwa mno kwamba baada ya kuzungumza na waandishi, Ole alimshutumu Sonny lakini ninyi hamkuniuliza hilo.”