Talaka zilivyowafilisi mastaa wa soka duniani

PARIS, UFARANSA. Hivi karibuni stori kubwa ni kumhusu mchezaji wa kimataifa wa Morocco anayeichezea PSG, Achraf Hakim ambaye ameandikisha mali zake zote chini ya jina la mama yake, hivyo mkewe ameambulia patupu baada ya kuwasilisha maombi ya talaka mahakamani.
Hakim ambaye alifunga ndoa na mkewe, Hiba Abouk mwaka 2020 wana watoto wawili kitendo chake kimekuwa funzo kwa wachezaji wengi.
Hapa tumekuletea wachezaji watano ambao walifilisika baada ya kuachana na wake zao na mali zao kukombwa jambo ambalo Hakim naye lingemkuta.


Emmanuel Eboue
Mmoja kati ya wachezaji ambao wameacha funzo kubwa kwa wachezaji wa Kiafrika, Eboue ambaye aliwahi kuichezea Arsenal kuanzia mwaka 2005 hadi 2011.
Alipoteza pesa zake na mali zake baada ya kuachana na mkewe Aurelie ambaye alizaa naye watoto watatu.
Eboue anasimulia pesa zote za usajili na mshahara alizokuwa anazipata alikuwa akimpa mkewe na kuna muda alikuwa anasaini makaratasi bila kujua kama alikuwa ni makubaliano ya kumrithisha mkewe mali zake.
Baada ya talaka Eboue akapoteza kila kitu na kurudi kwao Ivory Coast kuanza moja.
Hata hivyo, baada ya mahojiano yake, timu mbalimbali ikiwemo Arsenal na Galatasaray zilijitokeza na kumpa nafasi ya kufanya nao kazi kwa sasa yupo zake Ivory Coast ambako amefungua akademi ya kulea wachezaji ambao baada ya muda hupelekwa barani Ulaya.


Asamoah Gyan
Oktoba mwaka 2018, ripoti kutoka vyombo vya Afrika na Ulaya zilieleza mchezaji wa zamani wa Ghana, Asamoah Gyan amefilisika baada ya kuachana na mkewe na yeye mwenyewe akathibitisha amebakiwa na Pauni 600 tu kwenye akaunti yake ya benki.
Hata hivyo, staa huyu alishtuka mapema na kuanzia nyumba, magari na mali nyingine zote aliziandika chini ya jina la kaka yake hivyo akasalimika kwenye mtego huo.
Hata hivyo baada ya talaka Gyan aliomba watoto watatu aliozaa na mkewe Gifty wafanyiwe vipimo vya DNA ili kugundua ikiwa ni watoto wake kweli na kama sio nayeye adai fidia.


David James
Jamaa aliwahi kuwa golikipa wa Liverpool na Manchester City katika nyakati tofauti. Mwaka 2005, baada ya kuachana na mkewe, Tanya ambaye alianza uhusiano wa kimapenzi tangu wakiwa na watoto, umaskini ndio ukaanza kumuandama.
Talaka yake ilimgharibu Pauni 3 milioni ambayo ni zaidi ya 6 bilioni za Kitanzania.
Baada ya hapo akaanza kuuza baadhi ya vitu vyake vya ndani ikiwemo magari, jezi na vifaa vya mazoezi ili kupata pesa.
Rafiki yake wa karibu Stan Collymore anasimulia kwamba mbali ya talaka, James alikuwa akipoteza sana pesa katika matumizi ya kawaida.
“Hata alipokuwa amenunua gari jipya ikipata mkwaruzo kidogo tu, anaiweka uwani na kwenda kununua mpya, viatu alikuwa harudii, akishavaa anavitupa stoo na kununua vipya.”


Taribo West
Staa huyu raia wa Nigeria ambaye aliwahi kuzichezea Inter Milan na AC Milan kati ya mwaka 1997 hadi 2000, yeye pia alifilisika baada ya talaka na kwa sasa ameamua kuwa mchungaji kabisa.
Taribo ambaye alioana na Minigeria mwenzake Atinuke Ekundayo alipoteza pesa zake nyingi kwenye starehe zilizosababisha asiwe na maelewano mazuri na mke wake hali iliyosababisha mwana mama huyo kwenda mahakamani kudai talaka na fidia.


Paul Merson
Mchezaji huyu wa zamani wa Arsenal alikuwa na wakati mzuri kwenye kikosi hicho chini ya Arsene Wenger ambapo alifanikiwa kubeba taji la FA Cup ambalo kwa wakati huo ndio lilikuwa likitambulika kama taji la ligi.
Baada ya kukusanya pesa za kutosha wakati wa uchezaji wake, Merson alianza kuzipoteza pesa hizo kutokana tabia ya ulevi kupindukia na matumizi ya madawa yakulevya hali iliyosabahisha apoteze zaidi ya Pauni 3 milioni.
Baada ya hapo pesa nyingi pia ikapotea kam mgao baada ya kuachana na mkewe.
Hali hiyo ikasababisha auze hadi nyumba yake iliyopo England kwa ajili ya kulipa madeni.
Kwa sasa amerudi kwenye mstari kwani anafanya kazi kwenye Kituo cha TV cha Sky Sports kama mchambuzi wa soka.