Tatizo Yanga liko hapa

MASHABIKI wa Yanga wanakumbana na vitisho vingi vya kuwarusha roho kutoka kwa wapinzani wao kuwa zama zao zimepita na kwamba hata pale kileleni mwa msimamo walipokaa wamewashikia Simba.
Ni kweli kwamba Simba wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo na wako katika kiwango bora tena msimu huu wakifukuzia taji lao la nne ndani ya miaka minne.
Hii inachangia kujiamini zaidi na kuwakebehi Yanga kwamba wameshapotea katika ramani kiasi kwamba eti kati ya mashabiki 10 basi zaidi ya saba ni wa Simba.

Mikwara hii inawapandisha presha baadhi ya mashabiki wa Jangwani, lakini wanasahau kuwa takwimu hazipatikani kwa kuongea tu, bali vitendo.

Sampo ndogo ya uthibitisho kwamba Yanga bado haijatetereka katika suala la sapoti ni mahudhurio ya matamasha ya klabu mbili hizi zinazoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi.

Kila mmoja anakumbuka jinsi tamasha la Yanga lilivyofunika zaidi na kujaza zaidi mashabiki.
Simba imebakiza pointi nne kuwafikia Yanga walio na pointi 49 kileleni huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa na mechi mbili mkononi, ambazo Mnyama akishinda atakaa juu.

Na hapo ndio mbio za ubingwa wa nne mfululizo zitakaposhika kasi. Lakini Simba ikishinda ubingwa wa nne mfululizo ndo mwisho wa Yanga? Hapana.

Kwa sababu haitakuwa mara ya kwanza kwa timu kutwaa mataji manne mfululizo, historia inaonyesha.
Yanga ndio timu inayoongoza kwa kulibeba taji hilo mara nyingi mfululizo, ikilibeba mara tano mfululizo kuanzia 1968 hadi 1972 kisha Simba ikajibu kwa kulibeba mara tano mfululizo kuanzia 1976 hadi 1980.

Na kiujumla Yanga imelibeba taji hilo mara 25 na Simba mara 21.
Licha ya presha kubwa kutoka kwa Simba ambayo inatisha hadi Afrika sasa baada ya kuwakalisha watetezi wa taji la Ligi ya Mabingwa, Al Ahly ya Misri katika mechi yao ya Kundi A, Yanga wanataka kutunza heshima yao ya kuwa mabingwa wa kihistoria nchini.

Lakini kiwango cha timu yao katika siku za hivi karibuni kinawapa hofu mashabiki wao.

Timu haifungi mabao ya kutosha huku washambuliaji wake kama Mghana Michael Sarpong akilingana mabao na beki wao, Lamine Moro na Ditram Nchimbi akiwa hajafunga bao mwaka mzima.


TATIZO LIKO HAPA

Kinachotokea sasa Yanga ni kile walichoanza nacho msimu.

Timu ilikuwa na maingizo mapya mengi. Wachezaji saba au zaidi wanaoanza katika kikosi cha kwanza wamesajiliwa msimu huu huku pia wakibadilisha kocha katikati ya msimu, wakiachana na Mserbia, Zlatko Krmpotic na kumchukua Cedric Kaze wa Burundi.

Timu ilianza msimu kwa soka la jihadi, wachezaji walijituma na kucheza kwa morali ya juu. Ilikuwa ngumu kuwafunga chini ya ukuta ulioundwa na Lamine Moro, beki pekee wa kikosi cha kwanza aliyebaki kutokea msimu uliopita akishirikiana mapacha wake watatu wapya Bakari Nondo Mwamnyeto, Kibwana Shomary na Yassin Mustapha.
Kiungo cha nyota aliyetua msimu huu, Mukoko Tonombe kulifanya pacha makini na Feisal Salum na Deus Kaseke. Upambanaji wa kujituma na sakasaka ya mapafu ya mbwa viliwafanya Yanga kuwa timu ngumu sana kucheza nayo Simba wanatambua walichokutana nacho katika mechi yao ambayo Wekundu wa Msimbazi walishangilia sare siku hiyo. Ni baada ya beki Joash Onyango kusawazisha bao ‘usiiiku’ wakati watu wakidhani mabingwa wamelala siku hiyo katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza wa VPL Novemba 7, 2020.

Lakini licha ya kucheza kwa kujituma, Yanga tangu wakati huo haikuwa ikifunga mabao ya kutosha.

Mechi nne za kwanza za msimu huu walifunga mabao manne tu na walihitaji mechi tano ili kufunga zaidi ya bao moja kwenye mechi walipowalaza Coastal Union 3-0.

Hata hivyo, hadi kufikia mechi ya tisa walikuwa wamefunga mabao 11 tu, mechi 10 walikuwa na mabao 12 tu, hata katika mechi 12 walikuwa na mabao 15 tu.
Ushindi mkubwa ulikuja dhidi ya timu ya mkiani ya Mwadui waliyoifunga 5-0 na Saido Ntibazonkiza aliyesajiliwa katika dirisha dogo alipoanza kuitumikia, Yanga ilishinda kwa kujiamini 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na 3-0 dhidi ya Ihefu.

Ni kipindi hiki Yanga ilionekana kuwa tishio kwelikweli. Gari lilikuwa limewaka. Saido alithibitisha ni mtu ambaye alikuwa akikosekana Yanga. Hawakuwa na mtu anayecheza nyuma ya straika mwenye uwezo wa kupika mabao na kufunga.

Saido katika mechi mbili alizocheza alihusika moja kwa moja katika mabao matano akifunga mawili na kutoa asisti tatu. Uwapo wake uwanjani ulimfanya kila mchezaji ang’ae.

Alijua kuwachezesha kina Kaseke, Yacouba Sogne, Tuisila Kisinda, Sarpong na wengine wa mbele yake. Na sasa hayupo tatizo linajirudia. Na walio nyuma yake walicheza kwa kujiamini, kwavile walijua mpira ukifika kwake kuna jambo litatokea mbele na analifanya kiuhakika.

Yacouba akatengeneza pacha ya kutisha na Kaseke. Lakini tangu Saido ameumia, Yanga imerejea kule kule ilikoanzia. Haifungi mabao ya kutosha na inahaha sana uwanjani.

Inapokuwa na Saido na Yacouba wazima na katika ubora wao kikosini, Yanga inakupasua, lakini bila ya Saido Yanga haitembei. Yanga inawahitaji nyota hao kikosini. Zamani alikuwepo Mzimbabwe Thabaan Kamusoko maarufu kama kampakampa tena.

Kama itashindwa kuwapata kutokana na majeraha ya mara kwa mara kama ilivyo sasa, ni lazima isubiri dirisha lijalo isajili fundi wa eneo la kati ambalo kwa mahasimu wao Simba ni burudani tu kwa sababu wanaye Clatous Chama.

Ni lazima Yanga wawe na Saido aliye mzima katika ubora wake au wawe na Chama wao.

Kwa maoni tuma kwenye namba: 0658376417