The return of the Champions, kikosi kizima Yanga hiki hapa

MASHABIKI wa Yanga kwa sasa wanahesabu saa tu kabla ya kuona jeshi lao likishuka uwanjani kwenye mechi yao ya kwanza ya kimataifa tangu ilipocheza mara ya mwisho mwaka 2019.

Unaweza usiwaelewe wanayanga wanapotamba na kauli mbiu yao, ‘Return of the Champions’ ikiwa ni hamasa yao kuelekea mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu yaliyoanza juzi.

Hata hivyo, kuna sababu kadhaa zinaonekana zimewapa chachu Yanga hadi wakaamua kuibua na kutamba na kauli mbiu hiyo iliyotangazwa na Msemaji wao, Haji Manara waliyoamua kutembea nayo akilini kwa sasa wanaposhuhudia timu yao ikiikaribisha Rivers United ya Nigeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa.

Mara ya mwisho Yanga ilicheza mechi za kimataifa za CAF Septemba 28 walipofumuliwa mabao 2-1 na Zesco United katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutoka sare ya 1-1 nyumbani. Kama hufahamu, Yanga ndio timu ya kwanza hapa Tanzania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakifanya hivyo mwaka 1998 ingawa walimaliza wakiwa wa mwisho katika kundi lao lililokuwa na timu za Manning Rangers, Raja Casablanca na Asec Mimosas.

Pia Yanga sio wanyonge katika mashindano ya kimataifa kwani baada ya mwaka 1998, iliingia mara mbili katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016 na 2018, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na timu yoyote katika michuano hiyo licha ya Namungo kutinga nao msimu uliopita.

Kocha wao Nasreddine Nabi naye anawapa jeuri ya kutamba kuwa wamerejea kibingwa katika michuano ya CAF, kwani ameshawahi kuonja ubingwa wa Afrika akifanya hivyo mwaka 2012 alipoiongoza AC Leopards ya Congo kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika lakini pia ameshawahi kuiongoza Al Hilal ya Sudan kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Pia Yanga ndio timu inayoshikilia mataji mengi ya Ligi Kuu Bara ikiwa na 27 tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965.


KIKOSI CHA KIBABE

Yanga inaivaa Rivers pengine ikiwa na kikosi kilichosheheni idadi kubwa ya wachezaji wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa kulinganisha na miaka ya hivi karibuni ambayo hawakufua dafu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ducapel Moloko, Yannick Bangala, Heritier Makambo, Mukoko Tonombe na Djigui Diarra kwa nyakati tofauti wamecheza hatua ya robo fainali ama zaidi katika Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho la Afrika wakiwa na timu za AS Vita, Horoya na Stade Malien

Hata hivyo, Yanga kwa upande mwingine itakuwa na pigo la kuwakosa Khalid Aucho, Fiston Mayele na Shaban Djuma ambao hawatocheza hatua za mwanzoni baada ya hati zao za uhamisho wa kimataifa (ITC) kuchelewa kupatikana kabla ya muda wa mwisho wa kuziwasilisha uliopangwa na CAF. Lakini Yanga bado inao wachezaji wa kutosha wa kuiwezesha kupata matokeo mazuri leo kutokana na usajili ambao imefanya.

Kikosi cha Yanga katika mechi hiyo kinaweza kuundwa na wachezaji Djigui Diarra, Shomary Kibwana, Adeyoum Saleh, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mukoko Tonombe, Ducapel Moloko, Yannick Bangala, Heritier Makambo, Feisal Salum na Yacouba Songne. Kwenye benchi wanaweza kuwepo Erick Johora, Paul Godfrey, Yusuph Athuman, Abdallah Shaibu, Deus Kaseke, Zawadi Mauya na Ditram Nchimbi


MBINU KUIBEBA

Yanga kama itatumia vyema mashambulizi kutokea pembeni, inaweza kuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na udhaifu wa Rivers katika upande huo, japo timu hiyo ya Nigeria ipo imara zaidi katikati mwa uwanja. Hapana shaka, kocha Nabi wa Yanga ataanza na mfumo wa 4-2-3-1 ambao amekuwa akipendelea kuutumia tangu alipojiunga na timu hiyo.

Pia Yanga inapaswa kujipanga vilivyo zaidi katika kipindi cha pili kwani katika siku za hivi karibuni imekuwa na tatizo la kukata pumzi katika dakika 45 za pili za mchezo.


WASOMALI KUHUKUMU

Marefa wanne kutoka Somalia ndio wamepangwa na CAF kuchezesha mechi hiyo ya leo ambayo mashabiki hawatoruhusiwa kuingia uwanjani. Refa Hassan Mohamed Hagi ndiye atakayesimama katikati na atasaidiwa na Suleiman Bashir na Ali Mohamud Mahad huku refa wa akiba akiwa ni Ahmed Hassan Ahmed.

Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Lewis Madeleine kutoka Shelisheli huku Ofisa Vipimo wa Uviko-19 akipangwa Violet Michael Lupondo wa Tanzania.


TUMAINI LIPO HAPA

Tumaini la Kocha Nabi lipo kwa nyota wake Feisal Salum na Heritier Makambo aliyekuwa akiwanoa juzi kwa mara ya mwisho jinsi ya kutupia kambani.

Katika mazoezi yao yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Nabi alikuwa anawapa wachezaji hao jukumu la kuhakikisha wanafunga.

Nabi alipanga timu mbili ya kwanza ikiwa ni Diara Djigui, Kibwana Shomari, Adeyum Saleh, Bakari Mwamnyeto,Dickson Job, Yanick Bangala, Heritier Makambo, Feisal Salum na Yacouba Sogne.

Kikosi kingine Nabi aliwachanganya wachezaji wake Eric Johola, Paul Godfrey, Abdallah Shaibu, Zawad Mauya, Ditram Nchimbi, Farid Mussa, Dickson Ambundo, Fiston Mayele, Djuma Shaban.

Kwenye mazoezi hayo Nabi alikuwa anasimamia zaidi upande wa kikosi kilichokuwa kinaongozwa na kipa Djigui kwa umakini wa hali ya juu.

Kocha huyo aliwataka viungo wake Yanick Bangala na Tonombe Mukoko wawe wepesi kupeleka mashambulizi kupitia pembeni.

Mukoko na Bangala walikuwa wanatumia upande wa Moloko kupeleka mashambulizi huku Moloko spidi yake ilikuwa mkubwa na akisogea karibu na kupiga krosi na Makambo alikuwa na kazi ya kufunga huku mpira ukitoka nje ya boksi basi Feisal alikuwa anapiga mashuti.

Nabi alipoona Yacouba spidi yake ndogo kwenye kupeleka mashambulizi alimbadilisha na kumchukua Farid Mussa ambaye alionyesha utofauti na Yacouba kwenye kuumiliki na uharaka wa kupeleka mashambulizi.

Makambo na Feisal walikuwa wanacheza kwa maelewano mazuri na mmoja akiwa anatoka kwenye boksi basi mwingine anabaki.

Fei pia alikuwa anatumia silaha yake ya kupiga mashuti ya mbali jambo ambalo lilionekana kufurahiwa zaidi na kocha Nabi.

Wakati Yanga wakiwa wanafanya mazoezi wachezaji wengine Yassin Mustapha, Bryson Rafael nw Mapinduzi Balama wao walikuwa na programu maalum kwa pembeni.

Wachezaji hao ambao ni majeruhi walikuwa wanafanya zaidi mazoezi ya kunyoosha viungo vya mwili na kuuchezea mpira kidogo.


MSIKIE NABI

Licha ya kuwakosa wachezaji watatu tegemezi, Kocha Nabi kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza wapo tayari kwa mchezo huo

“Wachezaji waliorudi kutoka katika timu za taifa wote wapo vizuri na nitawatumia, ambao watakosekana kwa sababu mbalimbali kuna mbadala wao watacheza kwenye nafasi hizo.

“Nimewajengea hali ya kujiamini wachezaji wangu pamoja na kuwapa mbinu sahihi ya kupata ushindi ili kujirahisishia kazi katika mchezo wa marudiano, kwani tunacheza na timu ngumu ambayo tunaiheshimu kutokana na ukubwa wao,” alisema Nabi. Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo alisema wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanaitupa nje Rivers United na kufanya vyema katika mashindano hayo.

“Tunajua hizi mechi ni ngumu, lakini Yanga haijajiandaa kwa unyonge. Tupo tayari katika mikakati ya kushinda hasa hii mechi ya hapa nyumbani na sio kwa kubahatisha tunachotaka, ni kuona hizi mechi mbili tunamaliza kazi kubwa hapa nyumbani.

“Tunataka kushinda kwa ushindi mzuri usio na mashaka hapa nyumbani. Ni muhimu katika mechi za namna hii ukawa na faida ya kuweza kutumia hatua ya kuanzia nyumbani ili kule kwao usiwe na kazi ngumu na hiki ndicho Yanga itakachofanya,” alisema Gumbo. Mbali na mechi hiyo ya Dar, kule visiwani Zanzibar nako kutakuwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Mafunzo na Inter Clube ya Angola utakaochezwa kwenye Uwanja wa Amaan.