Ubishi wa Fei Toto,  Muda kumalizwa Amaan 

Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam na Mudathir Yahya wa Yanga, wote ni viungo wanaofanya vizuri katika timu zao ambazo leo Jumapili zinakwenda kucheza mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Mchezo huo ambao awali ulipangwa kuchezwa Karatu mkoani Manyara, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaona liuhamishe mpaka Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex. Hiyo ni kutokana na uwanja wa awali kutokidhi vigezo.

Baada ya fainali hiyo kupelekwa Zanzibar, ni kama imeibua vita kubwa baina ya mashabiki wa Fei Toto na Mudathir ambao kila mmoja ametamba upande wake utaibuka na ushindi.

Mwananchi limefanya mahojiano maalum na mashabiki hao ambao katika tambo zao zote, mwisho wa siku wameamua kwamba Uwanja wa New Amaan Complex ndiyo utatoa majibu sahihi ya nani mbabe.

Kutoka maeneo ya Kwa Alimsha, ndipo inapatikana maskani ya Fei Toto, hapa kuna marafiki na mashabiki wa kiungo huyo waliozungumza na kutoa tambo zao.

Mudrick Abdallah kutoka upande wa Fei Toto, anaanza kwa kusema: “Fei ninaishi naye mtaa mmoja, kitambo sana nimekua naye tangu kipindi tunacheza soka la visoksi, baada ya hapo akaenda kucheza timu moja inaitwa Criss ipo Jang’ombe, alicheza Juvenile, baadaye Central, akaonekana na JKU ikamchukua.

“Hivyo kutokana na ukaribu wangu na yeye, siku hiyo ya mechi nitakwenda uwanjani kwa ajili ya kumsapoti yeye na naamini atatupa furaha mashabiki zake na kuwanyamazisha upande wa pili.”

Abdulhamid Hamad ‘Ringe’ naye anasema: “Kiwango cha Fei mpaka sasa hivi kimerudi baada ya kupata matatizo alipokuwa Yanga kwani awali kama kilishuka kidogo, baada ya kumaliza stress zake anacheza vizuri.

“Wakati yupo kwenye matatizo na Yanga tulikuwa tunajisikia vibaya kwa sababu yule ni kama mwanetu akipata matatizo hapa maskani lazima tumpe mawazo ili mwenyewe apunguze stress. Baada ya kumpa mawazo, akafanya dua na jambo lake likaisha.

“Ameenda Azam kutafuta maisha na katika kutafuta maisha lazima utoke sehemu moja kwenda nyingine, ndiyo Fei amefanya hivyo. Yeye ni kama mwanangu, na nimekuwa nikimuombea aendelee kufanya vizuri na naamini atafanya kweli pale Amaan.”

Yumi Yusuf Mwinyi kwa upande wake anasema: “Fei mwanzo alikuwa na kiwango kizuri ndani ya Yanga lakini baada ya kupata yale matatizo kiwango chake kikapungua, lakini alipoenda Azam kiwango chake kimeongezeka mara mbili zaidi.

“Fainali ni kama fainali huwa haitabiriki, kwa maoni yangu fainali itakuwa ngumu lakini Fei ataonyesha kiwango bora, namtabiria kufungua bao katika mchezo huo.

“Hapa mtaani kwetu sisi ni mashabiki wa Fei, tutaenda uwanjani kwa wingi kumsapoti kijana wetu. Hatutamuacha peke yake.”

Saleh Jaffar ‘Turan’ kidogo amekuwa tofauti na wenzake kwani yeye ameamua kuweka mapenzi yake na Simba pembeni, ameamua kuungana kumshangilia Fei Toto.

“Tunatarajia Fei ataonyesha kiwango cha juu kwa sababu amerudi nyumbani, watu wengi tulikuwa tunamuombea dua baada ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine, tunaendelea kumuombea dua na Mungu amzidishie.

“Mimi ni shabiki wa Simba lakini katika mchezo wa leo Jumapili nitakuwa Azam kwa sababu tu ya uwepo wa Fei kwani kila mtu anakipenda cha kwao.”

Baada ya kuwasikia watu wa Fei Toto, upande wa Mudathir Yahya ambaye maskani yake inapatikana Jang’ombe Mzizima kwa Gangster, nao wametoa tambo zao.

Nabeel Mohamed Abdallah, anasema: “Mudathir ni kiungo chuma, akiwa kama mzawa wa Zanzibar na hapa ndipo alipokulia kwa Gangster. Ukija kumtafuta Mudathir fika hapa ndiyo maskani kwake.

“Zanzibar Greatest au Zanzibar Goat ndiye Mudathir, ni kiungo ambaye hana mfano wake wapo ambao watamfananisha na Fei lakini wajue kwamba hana mfano. Jumapili lazima awalaze watu na viatu.”

Saido Mapilau anabainisha kwamba: “Mchezo wa Jumapili tutamuombea dua tu Mudathir kwani simu yake imepatikana na alisema iliibwa Tandale. Kazi tushamaliza kabisa na Jumapili nitakuwepo uwanjani kumsapoti, naamini atafunga na kumaliza ubishi uliopo. 

“Ubishi upo tu lakini ukweli ni kwamba, hakuna kiungo wa kumfananisha na Mudathir. Yeye ndiyo baba lao hapa Zanzibar.”

Kwenye Ligi Kuu Bara, Mudathir amefunga mabao 9 na kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa, wakati Fei ambaye amekuwa katika kiwango bora kabisa cha maisha yake ya soka, amefunga ambao 19 na kuiwezesha Azam kufuzu ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kushika nafasi ya pili huku yeye pia akishika nafasi ya pili ya ufungaji bora nyuma ya Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyefunga mabao 21.